CHINA: MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM kutoka Shina la Shanghai, China. Wana-CCM ambao walifika kumpongeza kwa mafanikio ya miaka minne ya uongozi wake wa kuleta maendeleo ya kiuchumi, kuboresha sekta za kijamii, na kuendelea kuimarisha diplomasia ya kimataifa.
Akizungumza na wanachama hao wa CCM Shanghai nchini China,Rais Dk. Mwinyi amewashukuru Wana-CCM wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana, Shina la Shanghai kwa salamu zao za pongezi na kwa kutambua mafanikio ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake.
Rais Dk. Mwinyi amesema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kuwashirikisha Watanzania wanaoishi nje ya nchi pamoja na wengine wasio raia lakini wenye asili ya Kitanzania.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iko katika mchakato wa kuandaa sera maalum itakayowanufaisha wanadiaspora kwa kuwapa hadhi maalum itakayowapa fursa mbalimbali zinazofanana na zile zinazotolewa kwa raia wa Tanzania.
Amesema sera hii inalenga kuwapa wanadiaspora nafasi za kushiriki katika shughuli za kiuchumi, kijamii, na maendeleo ya nchi kwa karibu zaidi, huku ikiwajengea mazingira bora ya uwekezaji, umiliki wa mali, na ushirikiano wa karibu na Serikali.
SOMA: CCM: Wagombea uchaguzi mitaa msibweteke
Rais Dk. Mwinyi pia amewahimiza Vijana wa CCM kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.