DAR ES SALAAM: CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimewataka wagombea wateuliwa katika nafasi ya wenyeviti uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, kutobweteka kwani uchaguzi hautapita bila kupingwa.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa (CCM- NEC), Itikadi Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla ametoa agizo hilo leo Novemba 4,2024 alipozungumza na viongozi na wanachama wa chama hicho Wilaya ya Kinondoni ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tisa katika Mkoa wa Dar es salaam na Pwani.
Makalla amesema katika uchaguzi huu kuna watu wamesema wanahakikisha kuwa uchaguzi huu hauna kupita bila kupingwa kwa kutaka kuwashawishi wananchi wanapiga kura za hapana hata kama CCM ndiyo imeteuliwa.
“Wana CCM hatulali tuko imara kuhakikisha hata pale ambapo tupo pekee yetu tutafanya kampeni kuhakikisha wagombea wetu wanapata kura za ndio kwahiyo wanaosubiri watasubiri sana,” amesema Makalla.