UVCCM Taifa wapata mwenyekiti mpya
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umemchagua Mohamed Ali Mohamed maarufu Kawaida kuwa Mwenyekiti wa umoja huo taifa.
Msimamizi wa uchaguzi huo, Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson alimtangaza Kawaida mshindi kwa kupata kura 523 na Rehema Omary alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti kwa kupata kura 416.
Nafasi za Mwenyekiti na Makamu UVCCM taifa zilikuwa wazi kwa takribani miaka miwili baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM taifa, Hery James kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa UVCCM, Tabia Mwita Maulid aliteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Katika nafasi ya uwakilishi kutoka UVCCM kwenda Jumuiya ya Wazazi imechukuliwa na Shaban Shaban aliyepata kura 119.
Pia nafasi mbili za ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NECZanzibar) zimechukuliwa na Hussein Haji Ussi aliyepata kura 397 na Mwanaenzi Hassan Suluhu aliyepata kura 387.
Aidha, waliopata nafasi ya uwakilishi wa nafasi tatu za ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NECTanzania Bara) ni Lulu Mwacha aliyepata kura 472, Ramadhani Mwinshehe aliyepata kura 434 na Mussa Mwakitinya kura 402.
Nafasi tatu za ujumbe wa Baraza Kuu la Taifa Tanzania Bara zimechukuliwa na Shamira Mshangama aliyepata kura 358, Gloria Katalambula kura 232 na Jenipha Mamuhindo kura 139.
Baada ya kutangazwa mshindi, Kawaida alisema ni wakati wa kutambua vipaumbele vya kuendeleza uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na nchi za jirani, utawala bora, haki na usawa katika mambo mbalimbali.
“Hivyo UVCCM unatakiwa kuwa mstari wa mbele kumsaidia Rais Samia na Dk Hussein Ali Mwinyi katika kutimiza maono yao ya kuifanya Tanzania iwe moja ya nchi zinazoendelea kwa kasi,” alisema na kuongeza: “Niwaahidi UVCCM chini ya utawala wetu wa miaka mitano utakuwa wa kushirikiana, kushauriana na kusimamia vipaumbele vya nchi na utekelezaji wa ilani ya CCM kuanzia ngazi ya shina.” Kawaida alisema UVCCM si jumuiya lele mama hivyo katika kipindi cha miaka mitano ijayo watahakikisha inakuwa imara na kuzuia watakaotaka kuujaribu umoja huo, Muungano, mshikamano wao, mapinduzi ya Zanzibar, uhuru wa Tanzania na usalama wa taifa.
Alisema katika kipindi cha kampeni alitembelea zaidi ya mikoa 25 na kupokea malalamiko na ushauri na kwamba amesikia na kuona mengi zikiwamo changamoto za ofisi, ukosefu wa mafunzo na fursa za kujiendeleza, maslahi ya watendaji na fursa za ajira.
Makamu Mwenyekiti UVCCM, Rehema alisema mchakato wa uchaguzi umeisha hivyo alihimiza vijana wenzake wavunje makundi na kama walikwazana wasameheane ili kuijenga jumuiya kwa maslahi ya nchi.