Uwekezaji DP World waanza kuleta matunda

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa, amesema maboresho yaliyofanywa kupitia ushirikiano na sekta binafsi yameongeza ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam, hatua iliyochangia ukuaji wa mapato, kupunguza msongamano wa meli, na kuongeza ajira kwa Watanzania.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa TPA katika miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Mbossa amesema maboresho yaliyofanywa na DP World yamewezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuongeza makusanyo ya kodi hadi kufikia wastani wa Sh trilioni 1 kwa mwezi kwa mwaka wa fedha 2024/25, kutoka Sh bilioni 850 kwa mwaka wa 2023/24.
Pia, maboresho hayo yamepunguza msongamano wa meli, hasa katika msimu wa shehena nyingi (Septemba – Novemba 2024), ambapo wafanyabiashara waliweza kusafirisha mizigo yao bila kucheleweshwa.
Aidha, makampuni ya meli yameanza kupunguza gharama za usafirishaji, ikiwemo Kampuni ya MSC ambayo imeondoa tozo ya ziada ya Dola za Marekani 1,000 kwa kasha iliyokuwa ikitozwa kutokana na ucheleweshaji wa huduma.
Katika upande wa ajira, jumla ya Watanzania 779 wamepata ajira za moja kwa moja katika kampuni za uwekezaji zinazoendesha bandari, ambapo 299 wameajiriwa na DP World Dar es Salaam na 480 katika kampuni ya TAEGTL.
Mbossa amesema mafanikio haya ni sehemu ya juhudi za Serikali kuboresha sekta ya usafirishaji na kuhakikisha bandari inakuwa na tija zaidi kwa uchumi wa nchi



