Uzito uliokithiri, vitambi chanzo cha magonjwa yasiyoambukiza

Uzito uliokithiri, vitambi chanzo cha magonjwa yasiyoambukiza

WAKATI Watanzania na wadau wa masuala ya afya na lishe wakisubiri ripoti ya Utafi ti wa Afya ya Uzazi na Mtoto (THDS) na Utafi ti wa Kitaifa wa Lishe (TNNS) zote za mwaka 2022, yapo mambo makubwa matatu yanayoikabili sekta ya lishe ikiwemo uzito uliokithiri, viribatumbo au vitambi na udumavu.

Hii ni kwa mujibu wa utafiti wa lishe wa mwaka 2018 ambao ulibainisha kuwa wanawake ndio wanaoongoza kwa kuwa na viribatumbo kuliko wanaume kwani takwimu za THDS zinaonesha kuwa uzito uliokithiri umeongezeka kutoka asilimia 28 mwaka 2015 hadi asilimia 32 mwaka 2018.

Kwa upande wa kiribatumbo wanawake wanaongoza kwa kiwango cha asilimia 15 na wanaume asilimia 2.5.

Advertisement

Inaelezwa kuwa uzito uliokithiri ni moja ya viashiria vya ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo saratani, magonjwa ya moyo na kisukari.

Kwa upande mwingine, magonjwa hayo ya lishe yamekuwa fursa kwa wafanyabiashara wengi ambao huuza bidhaa zao kwenye mitandao ya kijamii wakieleza namna ya kupunguza tumbo na nyama uzembe hususani kwa wanawake.

Hivi sasa dawa zinazodaiwa kuondoa vitambi zinauzwa kila kona. Kama hiyo haitoshi, ‘diet’ ndio neno pendwa kwa wanawake huku wengi wao wakipata ushauri wa watu wasio wataalamu wa afya na kuwasababishia athari kedekede.

Hata hivyo, mapinduzi ya sayansi na teknolojia, kutofanya mazoezi na kutozingatia lishe bora kwa kula vyakula vyenye madini, vitamini, wanga na protini huchangia kwa kiasi kikubwa matatizo hayo.

Athari za kiuchumi pia hutajwa kusababisha ulaji usiofaa kwani huchangia upatikanaji wa vyakula vilivyoandaliwa kwa haraka, unywaji wa vimiminika vya viwandani na kutozingatia mazoezi.

Maadhimisho ya Siku ya Uzito Uliozidi na Kiribatumbo Duniani hufanyika Novemba 26, kila mwaka. Kwa mujibu wa utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO) uliochapishwa Juni 2021 kuhusu unene uliopitiliza, umebaini zaidi ya watu bilioni 1.9 wenye umri kuanzia miaka 18 wana uzito uliopitiliza na watu milioni 650 wana vitambi duniani kote.

WHO ilibainisha kuwa wanawake ndio wanaongoza kwa kuwa na vitambi kuliko wanaume kwa sababu ya asili ya miili yao kuwa na uwezo mkubwa wa kuhifadhi mafuta mwilini (excess fat).

Mganga Mfawidhi wa Nsambo Health Care Polyclinic, Dk Boaz Mkumbo anasema kitambi ni sukari ya ziada iliyohifadhiwa na homoni ya insulini katika mfumo wa mafuta kwani kadri hifadhi ya sukari inavyozidi mwilini ndivyo seli za mwili zinavyodumaa kitaalamu inaitwa insulin resistance.

Dalili za usugu wa homoni hiyo ni weusi shingoni na sehemu kwenye mikunjo, kuwa na mikunjo usoni na shingoni, hali ambayo inabadilisha damu na kuonesha kuwa homoni ya insulini ipo juu.

“Kitambi hakitokani na vyakula asili vya mafuta na si sehemu ya mwili. Madhara ya kitambi hutokana na muda ambao umeishi na mafuta ya ziada,” anasema Dk Mkumbo.

Anaeleza kuwa mwili haupendi mazingira ya sukari nyingi hivyo mwili hujiendesha salama kwa wastani wa gramu tano za damu na kwamba sukari yoyote ya ziada, mwili huifadhi.

Dk Mkumbo anasema homoni ya insulini kwenye damu muda wote inatakiwa iwe chini na hupanda pale tu mtu anapokula chakula endapo mtu atakuwa na lishe duni, homoni hiyo huwa juu hali inayosababisha homoni ya Testosterone kushuka na kuongeza uzalishaji wa homoni ya kike ya Estrogen.

Pia anasema kwa kawaida kitambi kinaathiri msukumo wa damu wa moyo ambao husukuma lita 5.6 za damu kila dakika (80mls kwa kila mdundo).

“Ukiwa na kitambi unapunguza uwezo wa moyo kufanya kazi ya ziada unakuwa na mapigo mabaya ya moyo, kupumua haraka haraka, ganzi mwilini, kuvimba miguu inayobonyea na kukosa pumzi unapotembea au kupanda ngazi.

“Hiyo ni dalili mojawapo ya mwili kuzidiwa maji ya ziada kwenye damu. Mtu mwenye uzito mkubwa homoni inayohifadhi na kushikilia mafuta na inayozuia chumvi na maji visitoke, hushindwa kufanya kazi hiyo na badala yake huzidisha kumimina ndani ya damu yako,” anasema Dk Mkumbo.

Kwa upande wake, Ofisa Utafiti wa Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Walbert Mgeni anasema kuwa katika utafiti walioufanya mwaka 2018, kulingana na kipimo cha Body Mass Index (BMI) kinacholinganisha kati ya urefu na uzito ulibaini kwamba asilimia 7.3 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 ni wembamba au wana uzito pungufu kiwango ambacho ni cha juu ukilinganisha na mwaka 2014.

Anasema asilimia 10 ya wanawake waliobainika kuwa na uzito pungufu ni kutoka Unguja Kaskazini, Pemba, Manyara, Kagera na Singida.

Kwa mujibu wa TNNS 2018, asilimia 31.9 ya wanawake wana uzito uliokithiri ambayo inaonesha ongezeko kutoka asilimia 29.7 mwaka 2014.

Kiribatumbo kimeongezeka kwa asilimia 20. Mgeni anasema kuwa mikoa inayoongoza kwa kuwa na wanawake wenye uzito uliokithiri na viribatumbo ni Kilimanjaro, Dar es Salaam, Mwanza na Kusini Unguja (Zanzibar).

“Uzito uliokithiri ni moja ya viashiria vya ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo ugonjwa wa moyo, saratani na kisukari. Lazima tuhakikishe lishe bora inazingatiwa kwa kuendelea kutoa elimu ili kupunguza magonjwa yanayoambukiza ambayo yanaligharimu taifa na familia kwa ujumla,” anasisitiza.

Mkazi wa Dar es Salaam, Princess Dominic, anasema hakuna siri kubwa ya kufuata katika maisha kama lishe bora. Anasema kuwa kufanya mazoezi ya kupunguza mwili hususani kitambi bila kuzingatia lishe ni kazi bure hivyo ili mtu aone mafanikio ya mazoezi anayofanya kwa ajili ya kupunguza uzito, anatakiwa kufuata lishe bora.

“Baada ya kujifungua niliongezeka kilo hadi kufikia 110 na hata umbo langu lilibadilika sikuvutiwa nalo, kuna wakati nilikuwa natumia mkanda wa kupunguza tumbo ili ninapokwenda kwenye matukio mbalimbali ya sherehe nionekane nimependeza. “Sikuwahi kuzingatia masuala ya lishe kwani chakula changu pendwa ni chipsi mayai, mishikaki na pepsi baridi, hali ilikuwa mbaya baada ya muda nilianza kutafuta watu wanaotangaza dawa za kupunguza mafuta na uzito kwa haraka ingawa gharama zake ni ghali lakini nilinunua ili kutimiza azma yangu ya kupunguza mwili, anaeleza Princess.

Anasema alitumia dawa nyingi ambazo nyingine zilimsababishia kuharisha kama ambavyo wataalamu hao walimuelekeza, alianza ‘diet’ lakini alishindwa kuendelea ndipo daktari alimwelekeza kufuata lishe bora ndipo alipata matokeo.

Jesika Sauli anasema kuwa tangu alipoacha kutumia vyakula vyenye wanga, mafuta mengi na sukari ame- punguza mwili wake kwa hara- ka na kwamba ataendelea kuzingatia ulaji unaofaa sambamba na kuelekeza familia yake ili kuepuka magonjwa.