DAR ES SALAAM: RAIS wa Shirikisho la mpira wa miguu la Tanzania (TFF), Walace Karia amesema Teknolojia ya Usaidizi wa Muamuzi kwa njia ya Video (VAR) inasubiri vibali kutoka katika idara ya VAR ya Shirikisho la mpia wa miguu la Kimataifa (FIFA) ili ianze kutumika rasmi katika ligi kuu ya Tanzania Bara.
Akizungumza kando ya hafla hiyo ya uzinduzi iliyofanyika katika Uwanja wa Benjamin mkapa jijini Dar es Salaam, Karia amesema tayari kuna ‘VAR kits’ mbili mpaka hivi sasa moja kutoka Shirikisho la mpira wa miguu Afrika (CAF) ambayo itafungwa katika uwanja huo na nyingine kutoa azam media ambayo ni ‘mobile’ inayohamishika.
“Ni kosa kutumia teknolojia hii bila kibali, kwakuwa ni jambo jema tumeomba vibali FIFA kwenye idara inayoshughulika na VAR ili waweze kuturuhusu kutumia kwenye ligi. Hii kutoka CAF ni ya mafunzo na tunanufaika moja kwa moja na uwepo wake kwa sababu uwanja huu ndio kituo cha mafunzo ya VAR kwa kanda ya CECAFA (Shirikisho la mpira wa miguu Afrika Mashariki),” amesema.
SOMA: ‘Wasiotimiza vigezo vya uwanja bora, wawekeni pembeni’
“Hii ya azam ni mobile VAR inaweza kwenda popote kwahiyo tukipata kibali hata kesho tutaanza kutumia kwenye ligi,” ameongeza.
Kuhusu ni viwanja vipi na mechi zipi hasa teknolojia hiyo itatumika, Karia amesema ikiwa watapata kibali, mechi zote zitakazochezwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa zitatumia teknolojia hiyo na mechi zingine zozote ambazo zitavuta hisia za watu wengi au zitakazo hitaji usaidizi wa VAR.
“Bado hatujaamua ni mechi ipi na ipi VAR itatumika, lakini ni uhakika kuwa mechi zote zitakazochezwa Benjamin Mkapa zitatumia teknolojia hii kwa sababu VAR kit hii kutoka CAF itafungwa hapa, kwakuwa ile ya azam media ni mobile inaweza kutumika kokote kwenye mechi yeyote ambayo inaonekana kuvuta hisia za watu wengi au yenye uhitaji ” amesema Karia.
Teknolojia ya VAR ilianza rasmi kutumika mwaka 2016 na leo Tanzania imeweka historia ya kuwa nchi ya kwanza Afrika Mashariki kumiliki teknolojia hiyo na iwapo itapewa kibali basi itakuwa nchi ya kwanza ukanda wa Afrika Mashariki na Kati yenye ligi inayotumia VAR.