Vesterbacka kufungua kituo cha kifinnish

DAR-ES-SALAAM : MWANZILISHI wa Kampuni ya Finest Future, Peter Vesterbacka, ametangaza mpango wa kuanzisha kituo cha kufundisha lugha ya Kifinnish hapa nchini Tanzania, hatua inayolenga kuwawezesha watanzania wengi kupata fursa ya kujiunga na mfumo wa elimu bure nchini Finland.

Vesterbacka, akieleza juu ya fursa hizo za elimu bure, alisema kuwa mfumo wa elimu wa Finland unatoa nafasi bora kwa kila mtu kuendelea na masomo yao, kuanzia ngazi ya sekondari hadi vyuo vikuu bila malipo.

“Ningependa kuona angalau watanzania zaidi ya elfu moja wakihudhuria masomo nchini Finland kupitia fursa ya elimu bure. Tafiti zinaonyesha kuwa watanzania zaidi ya elfu tatu wanakwenda kusoma mataifa mengine, kwa nini wasichague Finland?” aliongeza Vesterbacka.

Pamoja na mpango wa elimu, Vesterbacka alibainisha kuwa kufunguliwa kwa kituo cha kufundishia lugha ya Kifinnish kutasaidia kupunguza gharama kwa watanzania wanaotaka kuingia katika mfumo wa elimu bure wa Finland. Alisema,

“Kweli, tunapanga kufungua kituo cha kufundisha lugha ya Kifinnish, lakini bado tupo kwenye majadiliano.”

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya ExamNet Tanzania, Rodgers Mbaga, aliongeza kuwa fursa hii itawapa watanzania uwezo wa kufanya kazi na kusoma nchini Finland, kutokana na mahitaji makubwa ya wafanyakazi nchini humo.

“Finland ina idadi ndogo ya watu, takriban milioni tano na laki tano, na hivyo huduma zinazotolewa kwa kulipa kodi zinahitaji wafanyakazi. Watu wengi nchini Finland hawazaani kwa wingi,” alisema Mbaga.

Mbaga aliongeza kuwa hitaji la ongezeko la watu katika soko la ajira nchini Finland linakadiriwa kufikia watu 30,000 kwa mwaka, hali inayochochea upanuzi wa nafasi za ajira.

SOMATanzania yapata elimu bure ya Finland

 

Habari Zifananazo

Back to top button