Tanzania yapata elimu bure ya Finland
DAR-ES-SALAAM : TANZANIA ni miongoni mwa nchi zilizonufaika na mpango wa elimu bure wa Finland, ambapo hadi sasa wanafunzi zaidi ya 15 wamepata faida.
Mpango huu unahusisha ngazi zote za elimu, kuanzia sekondari, ufundi, hadi vyuo vikuu, huku watanzania zaidi ya kumi wakiwa wamenufaika hadi sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar-es-Salaam, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya ExamNet Tanzania, Rodgers Mbaga, amesema serikali ya Finland kupitia Finest Future imeanzisha mpango huu wa elimu bure ili kuwasaidia Watanzania kupata ujuzi na utaalamu katika fani mbalimbali.
“Hapa Tanzania na nchi nyingine za Afrika, zitapatiwa mwongozo wa mpango huu wa elimu bure kupitia ExamNet Tanzania, ambayo itatoa usaidizi kamili kuanzia usajili hadi maandalizi,” alisema Rodgers.
Mbaga aliongeza kwamba mwombaji atapata fursa ya kufanya kazi wakati wote wa masomo. “Wenzetu Ulaya wanaweza kusoma huku wakifanya kazi, tofauti na sisi. Fedha zao ni nzuri sana, hivyo unaweza kujihudumia bila shida yoyote,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Vyuo Vikuu vya Nje nchini Tanzania, Tony Kabetha, amesema kuwa Tanzania imekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na nchi za Ulaya, ikiwemo Finland, ambayo ina fursa nyingi za elimu.
“Finland ni nchi iliyopiga hatua kubwa katika sekta ya elimu na teknolojia ya mawasiliano. Tunapaswa kuchangamkia fursa hii,” alifafanua Kabetha.
SOMA Wanafunzi wapewa kompyuta 50 bure kukuza TEHAMA
: Mpango wa fursa ya elimu bure wa Finland umepangwa kuzinduliwa Jumamosi hii na Kampuni ya Finest Future kutoka Finland kwa ushirikiano na ExamNet Tanzania, ambao ni waratibu wakuu wa mpango huu.