Vifo huduma za dharura vyapungua asilimia 40

DAR ES SALAAM: HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) kupitia Kitengo chake cha Huduma za Dharura, imefanikiwa kupunguza vifo vinavyotokana na huduma hizo kwa asilimia 40, hali iliyochangia pia kupungua kwa malalamiko ya wagonjwa na kuboreshwa huduma kwa ujumla.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurungenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Mohamed Janabi wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Huduma za Dharura yaliyofanyika hospitalini hapo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dk Julieth Magandi amesema tangu kuanzishwa kwa huduma hizo mwaka 2010, MNH imekuwa kinara katika utoaji wa huduma bora za dharura nchini.
“Tangu kuanzishwa kwa huduma hizi, idara hii ni ya kwanza kutoa huduma za dharura nchini. Tumeweza kupunguza vifo kwa asilimia 40, na sasa tunatoa huduma hizi hadi nje ya hospitali,” amesema Dk Magandi.

Aidha, alitoa wito kwa wahudumu wa kitengo hicho kuwa tayari kutoa huduma wakati wote, kutokana na mahitaji makubwa ya jamii, hususan kwa wagonjwa wa magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza.
Ameongeza kuwa hadi sasa MNH ina idara 100 zinazotoa huduma mbalimbali zikiwa na vifaa tiba vya kisasa, huku lengo kuu likiwa ni kuhakikisha huduma za dharura zinapatikana kwa urahisi hata kwa kutumia simu ya mkononi.
ZAIDI SOMA:
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), anayeshughulikia Taaluma, Profesa Emmanuel Balandya amesema kwa mwaka 2024 chuo hicho kimeandikisha wanafunzi 48 wanaosomea huduma za dharura, watakaotumika pia kutoa huduma hizo wakati wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yanayotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Akitoa taarifa ya shughuli zilizofanyika kabla ya Kilele,Dk Humphrey Medarakini amesema katika kuadhimisha siku hiyo, huduma mbalimbali zimetolewa kwa wahudumu wa afya na jamii kwa ujumla, ambapo zaidi ya watu 170 wamepatiwa elimu kupitia mikutano ya hadhara na njia nyinginezo.
“Huduma za dharura zinazotolewa kwenye jamii kwa sasa zina uwezo wa kuokoa maisha kwa asilimia 50, jambo linalothibitisha mafanikio ya elimu na mafunzo tunayotoa,” amesema Dk Medarakini.




