Vigogo waharibifu wa mazingira kikaangoni

Makamu wa Rais Dk Philip Mpango

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amesema baadhi ya viongozi nchini kwa maslahi binafsi wanachangia uharibifu wa mazingira na ametoa maagizo matano katika kusimamia udhibiti wa uharibifu huo.

Pia ametaka apelekewe majina ya familia 12 na viongozi wakiwamo mawaziri, wanasiasa, wabunge na majaji wanaotuhumiwa kwa uharibifu katika Bonde la Usangu mkoani Mbeya.

Dk Mpango amesema hayo jana katika ufunguzi wa kongamano la wahariri na wadau wa uhifadhi, mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji lililofanyika hapa jana.

Advertisement

“Bahati mbaya kuna kundi la viongozi kwa maslahi binafsi wanachangia sana katika uharibifu wa mazingira,” alisema.

Aliongeza: “Mimi najiuliza kule hifadhi wale ng’ombe zaidi ya 3,000 ni wa mfugaji masikini au yale macombine harvest makubwa ni ya wakulima wale ninaowafahamu mimi, masikini kama mimi ninayetoka familia masikini.” “Hawa (viongozi) ndio wale niliosema wanywe sumu, kwa sababu wametanguliza maslahi binafsi kiasi kwamba mito kama Ruaha imekauka.” Alisema kutokana na uharibifu huo wa mazingira, “mazingira sasa yanalipa kisasi na tumeanza kulipa jeuri yetu.”

Aliongeza kwamba viongozi wa aina hiyo hawafai kwa sababu madhara yao ni makubwa kwa Watanzania. Akizungumzia madai ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile kwamba kuna familia 12 na viongozi mbalimbali waliovamia Bonde la Usangu, Makamu wa Rais aliagiza akabidhiwe orodha hiyo.

“Nilipojitosa katika vita hii nilijua kuwa si vita rahisi, lakini tumedhamiria, tutashinda vita hii.“Hayo majina nitaomba nikabidhiwe na kwa kuwa nchi hii inaendeshwa kwa haki na sheria, tutaenda kuyafanyia kazi ili kutoa haki,” alisema.

Aliagiza watendaji wa mabonde ya maji nchini kuanza kuchukua hatua dhidi ya wale wote waliovamia maeneo ya uhifadhi wakiwamo waliojenga kuta katika kingo za maji za Mto Ruaha Mkuu.

“Chukueni hatua sasa, chukueni hatua leo. Bomoeni kwa gharama zao, wale wenye vibali ambao pia wameweka vizuizi, nataka kuviona mniletee,” alisema.

Ameagiza apelekewe tathmini ya matumizi ya ardhi ambayo aliiagiza ili kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira nchini.

Aidha, ameagiza kukamilishwa haraka kwa kazi ya kuweka mipaka ya Ruaha. Kwa upande wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, aliwataka watii agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu mikakati ya sekta hiyo kuchangia kukuza uchumi, akisema sekta ya mifugo haina mikakati inayoeleweka.

Amemtaka Waziri Mkuu kumpa taarifa ya utekelezaji wa agizo lake kwa mikoa hivi karibuni kuhusu upandaji miti rafiki wa mazingira.

Katika maagizo yake sita ya jumla, Makamu wa Rais amewataka wanahabari nchini kuelimisha jamii kuhusu masuala ya mazingira na athari zake kwa nchi na kufanya habari za kiuchunguzi juu ya mazingira ili kuwafichua waharibifu wa mazingira. Katika agizo lake la tatu ni kuwapo kwa elimu linganifu ya ikolojia ikiwamo elimu ya uraia ya mazingira.

Dk Mpango pia ameagiza Watanzania wachangamkie fursa za utunzaji mazingira ikiwamo biashara ya hewa ukaa, akitolea mfano wa Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi inayovuna fedha nyingi.

Agizo lake la tano ni kumuunga mkono Rais Samia katika uwekezaji na utalii katika nchi hasa kwa sasa katika mikoa ya Kusini mwa Tanzania ambako kuna fursa nyingi. Awali, Mwenyekiti wa Kituo cha Wanahabari Watetezi wa Rasilimali na Taarifa (MECIRA), Habib Mchange alisema wanahabari wako tayari kuungana naye katika kudhibiti uharibifu wa mazingira. Mchange ambaye taasisi yake imeandaa kongamano hilo, alisema wanahabari “wako tayari kunywa sumu”, hatutakuachia jukumu hili peke yako.”

Akitoa mada kuhusu usimamizi wa ardhi oevu ya Usangu katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Kamanda wa Uhifadhi Ruaha, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Godwell ole Meing’ataki alisema Bonde la Ihefu limevamiwa na kwa siku 130 sasa halitiririshi maji kwenda katika vyanzo vya kufua umeme na uzalishaji.

Alisema kuna watu wamejenga kuta kuzuia maji hayo na wafugaji wamevamia bonde hilo na sasa hali ni mbaya.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *