Vijana, wanawake kunufaika kiuchumi mradi wa BRAC

IRINGA: Mamia ya wasichana, wanawake na vijana mkoani Iringa wanatarajiwa kujenga maisha mapya ya kujitegemea kiuchumi baada ya kunufaika na vifaa vya ujasiriamali vilivyotolewa na Mradi wa BRAC Maendeleo, hatua inayolenga kuwaondoa kwenye utegemezi na kuongeza uwezo wao wa kujipatia kipato.
Vifaa hivyo, vinavyojumuisha mashine za kushonea, vifaa vya saluni, sabuni, mafuta na vifaa vingine vya kuanzishia biashara ndogondogo, vimetolewa kama mtaji wa awali ili kuwawezesha wanufaika kuanzisha au kupanua shughuli zao za kiuchumi na kuboresha ustawi wa familia zao.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Meneja wa Mradi wa BRAC Maendeleo Tawi la Kihesa, Agnes Nchimbi, alisema uwezeshaji huo ni sehemu ya mkakati wa shirika hilo wa kuwainua wasichana na mama vijana kwa kuwapatia fursa za kujitegemea badala ya kutegemea misaada.
Alisema changamoto za kiuchumi zimekuwa zikiwakwamisha wasichana wengi na mama vijana kutimiza ndoto zao, hivyo utoaji wa vifaa hivyo unalenga kuwapa mtaji wa kuanzisha shughuli zenye tija na kuongeza kipato kwa njia endelevu.
“Tunataka wanufaika hawa wawe wajasiriamali wenye uwezo wa kujitegemea, kukuza biashara zao na kuboresha maisha yao pamoja na familia zao,” alisema Nchimbi.

Kwa upande wake, Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Iringa, Paul Mpwehe, aliwataka wanufaika kutumia vifaa hivyo kwa malengo yaliyokusudiwa ili viwe chanzo cha uzalishaji na si mali za matumizi binafsi.
Alisema fursa hiyo itakuwa na manufaa makubwa endapo vikundi vitasimamia vizuri vifaa hivyo, kufanya kazi kwa ushirikiano na kuhakikisha vinaongeza thamani ya biashara zao na kipato cha kaya.

Naye Afisa Maendeleo wa Kata ya Kihesa, Rebecca Lugenge, aliwahimiza wanufaika kuvitunza vifaa walivyokabidhiwa na kuvitumia kwa nidhamu ili viwe chachu ya maendeleo yao ya kiuchumi.
Alisema wanawake na wasichana wanapowezeshwa kiuchumi hunufaika si wao pekee, bali pia familia na jamii inayowazunguka kupitia ongezeko la kipato, ajira na ustawi wa kaya.

Baadhi ya wanufaika walieleza kuwa msaada huo umewapa matumaini mapya ya kujenga biashara zitakazowawezesha kujitegemea na kukidhi mahitaji ya familia zao.
Walisema wengi wao walikuwa na ujuzi wa kushona nguo, ususi na shughuli nyingine za ujasiriamali lakini walikosa mtaji wa kuanza kazi, hivyo vifaa walivyopokea vitawasaidia kugeuza ujuzi wao kuwa chanzo cha kipato.




F8BET thương hiệu giải trí cùng worl cup 2026