Vijana wanne watua Spain vipaji vya soka

VIJANA wanne wamechaguliwa na kupelekwa nchini Spain kwa ajili ya kuendelezwa kisoka baada ya kuonesha vipaji katika mashindano ya Kiruswa Jimbo Cup yaliyofanyika wilayani Longido, Mkoa wa Arusha.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Madini na Mbunge wa Longido, Dkt Stephen Kiruswa, kabla ya mchezo wa fainali ya mashindano hayo kati ya Mairowa FC na Olmoti, uliochezwa katika Uwanja wa Polisi Longido.
Kiruswa amesema anajivunia mafanikio ya mashindano hayo, akieleza kuwa ataendelea kuunga mkono jitihada za kuibua na kukuza vipaji vya vijana wilayani humo ili waweze kuendelezwa kisoka.
Amesema michezo ni chanzo cha afya, ajira na burudani, hivyo anaamini kuwekeza katika michezo kutasaidia vijana kutumia vipaji vyao kujenga maisha yao na kuliletea taifa mafanikio.

Amesema Kiruswa Jimbo Cup imefanyika kwa mara ya sita na amewataka wasimamizi wa mashindano hayo kuendelea kujituma kwa maslahi ya wananchi wa Longido na vizazi vijavyo.
“Nawashukuru sana wasimamizi wa mashindano hayo kwani wametimiza wajibu wao kikamilifu. Kama kuna mapungufu basi ni kidogo na yanaweza kurekebishwa mwakani,” amesema Kiruswa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Wilaya ya Longido (LDFA), Obeid Mollel, amesema lengo la mashindano hayo limeanza kutimia baada ya vijana wanne kufanikiwa kwenda Spain kwa ajili ya kuendelezwa zaidi kisoka.
Mollel amempongeza Kiruswa kwa jitihada za kuibua vipaji vya soka Longido, akisema hatua hiyo imewarahisishia wao kama wasimamizi wa soka katika wilaya hiyo kutekeleza majukumu yao.
Amesema mashindano hayo yalishirikisha timu 54 kutoka tarafa zote nne za Jimbo la Longido, huku Olmoti ikitwaa ubingwa baada ya kuifunga Mairowa kwa penalti 7-6.
Kwa ushindi huo, Olmoti ilijinyakulia Sh milioni mbili, mpira na seti moja ya jezi, huku Mairowa iliyomaliza nafasi ya pili ikipata Sh milioni 1.5 pamoja na mpira.
Mshindi wa tatu alipata Sh milioni moja, wakati timu iliyomaliza nafasi ya nne ilipata Sh500,000.
Mgeni rasmi katika fainali hiyo, Afisa Michezo wa Mkoa wa Arusha, Mwamvita Onoka Okeng’o, amempongeza Kiruswa kwa kuendelea kuandaa mashindano hayo, akisema yamekuwa sehemu ya kuwawezesha vijana kupata ajira na fursa za kuendelezwa kisoka ndani na nje ya nchi.

Okeng’o amesema vipaji vya kiwango cha wachezaji wakubwa duniani vinaweza kuwepo katika vijiji vya Longido, kinachohitajika ni usimamizi na uwekezaji mzuri ili vijana hao waweze kufikia ndoto zao.
Naye Katibu wa Mbunge wa Longido, Nai Nai, amesema mwakani mashindano hayo yatafanyika kwa ubora zaidi, huku kamati ikiwa na mpango wa kuboresha zaidi maandalizi na uendeshaji wake.



