Vijana watakiwa kuomba mikopo ya pikipiki

DAR ES SALAAM. VIJANA wametakiwa kujitokeza kuomba mikopo ya vyombo vya usafiri, ili kujikwamua kiuchumi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya MeTL na Mo Finance, Fatema Dewji alipokuwa akizindua rasmi kampuni ya mikopo Mo Finance itakayokuwa ikitoa mikopo ya pikipiki na bajaji.
Amesema wamegundua vijana wengi katika biashara ya kusafirisha abiria kwa bajaji na bodaboda wanakabiliwa na changamoto ya umiliki wa vyombo hivyo, hali iliyofanya kampuni yao kuja na wazo la kuwakopesha ili kusaidia kuwainua kiuchumi kwa kuwa na vyombo vyao wenyewe.
“Kupitia kauli mbiu ya Mo Finance ya ‘Kukuwezesha kwenye Uhuru wa Kifedha’, tumelenga kuwakwamua kiuchumi vijana wengi wa mtaani kupitia mikopo hii itakayozalisha ajira nyingi nchini,” amesema.
Amesema hiyo ni ya kwanza kwa kampuni yao kujihusisha na mikopo, huku akisisitiza hakujawahi kuwa wala hakuna kampuni nyingine yoyote kwa jina la MeTL inayotoa mikopo ya aina nyingine yoyote.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Madereva na wamiliki Pikipiki Mkoa wa Dar es Salaam (CMPD), Michael Massawe amesema wamefurahishwa na uzinduzi huu, ambao utasaidia kupunguza uhalifu mitaani, kwa kuzalisha ajira nyingi zaidi.