Vijana,watoto waathirika zaidi vifo vya kuzama maji

DAR ES SALAAM: UTAFITI uliofanywa na jumuiya za wavuvi katika mwambao wa Ziwa Victoria uligundua kuwa zaidi ya watu 217 kati ya 100,000 hupoteza maisha kila mwaka wakati wa kuvua ambapo asilimia 87 ya wanaopoteza maisha ni watu wazima ambao ndiyo nguvu ya taifa katika uzalishaji mali.

Aidha Takwimu zinaonyesha kuwa kila mwaka zaidi ya watu 235,000 duniani hupoteza maisha kutokana na matukio ya kuzama maji.

Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa serikali jana jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kitaifa kwaajili ya kujadili na kuandaa mpango mkakati wa kuzuia kuzama maji nchini Mkurugenzi wa huduma za kinga Wizara ya afya, Ntuli Kapologwe amesema takwimu hizo pia zinaonyesha kuwa wanaoathirika zaidi katika matukio hayo ni watoto na vijana, huku ikionekana zaidi ya asilimia 90 ya vifo hivyo vikitokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati.

“Suala la kuzama maji ni tatizo linaloathiri jamii yetu na kuwa tishio kwa maisha ya watu hususani watoto, wavuvi, wasafiri wanaotumia usafiri wa maji na hata wale wanaoishi karibu na fukwe na kuzama maji ni miongoni mwa majanga yanayoonekana kutokea mara kwa mara, nakuongezeka kwa kasi kubwa hivyo tunajadilia suala hili kwa kina ili tuchukue hatua .

Ntuli amesema ni muhimu kutambua kuwa kuzama maji ni tatizo linaloweza kuzuilika kwa kuchukua hatua kuhakikisha kuwa usalama wa wanaojihusisha na shughuli za maji kama vile kuogelea, uvuvi, au usafiri wa majini wanakuwa salama.

Amebainisha kuwa Ili kuweza kufanikisha suala hilo elimu juu ya hatari za maji na mafunzo ya uokoaji ni muhimu sana.

“Pamoja na hayo ni lazima kuendeleza programu za kuzuia kuzama maji kulingana na mapendekezo ya Shirika la Afya Duniani, unaosisitiza uwekezaji wa vizuizi, usimamizi, ujuzi wa kuogelea, mafunzo ya uokoaji pamoja na kudhibiti usafiri wa majini.

Aidha amesema jamii inapaswa kuwa na uelewa kuhusu sheria na kanuni za usalama majini na namna ya kutumia vifaa vya kuzuia kuzama maji kama vile majaketi ya kuogelea pamoja na namna ya kufanya uokozi endapo kutatokea kuzama maji.

“Ili kuweza kufanikisha haya yote kwa kuhakikisha jamii yetu inakuwa salama kwa kuzuia kuzama maji, ninawaomba tuendelee kutoa kipaumbele cha elimu kwa jamii juu ya usalama majini na mafunzo ya uokoaji.

Ntuli amesema Mpango Mkakati utasadia nchi na wadau mbalimbali kutenga rasilimali na nguvu katika maeneo muhimu ya kuzuia majanga ya kuzama maji na kupunguza vifo.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button