Vikundi 19 Babati vyakopeshwa

HALMASHAURI ya Mji wa Babati mkoani Manyara imekabidhi hundi ya zaidi ya Sh milioni 200 kwa vikundi 19 vya vijana, wanawake na makundi maalum.

Fedha hizo zimetokana na vyanzo vya mapato ya ndani ya halmashauri ya asilimia 10 zinazolenga kutoa mkopo usio na riba kwa wajasiriamali wadogo ili kujiinua kiuchumi.

Akikabidhi hundi katika ukumbi wa mkutano wa jengo la halmashauri hiyo wilayani Babati mapema leo, Mkuu Wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Kaganda amesema lengo ni serikali kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa.

Advertisement

Anasema kupitia waasisi wa taifa ambao vita kuu ilikuwa ni kupigana na umasikini, ujinga na maradhi vita ambavyo vinaendelezwa na uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan lengo kuu ni kuweka misingi ya taifa kiuchumi na uongozi bora.
“Tunapokwenda kujenga uchumi wa wilaya yetu, uongozi imara ni nyenzo muhimu ya kufikia uchumi wa kati ina maana hata mikopo itaongezeka kwasababu ya makusanyo yatakayopatikana,”

“Tukijenga uchumi wetu vizuri tukafungua sekta za utalii,kilimo na kuwa fedha zilizotolewa sio sadaka bali ni mkopo ambao kila mjasiriamali anapaswa kulipa kama sehemu ya takwa la kisheria kwakuwa mkopo ulitolewa kutokana na kukidhi vigezo na sifa za kutambulika kisheria,” amesisitiza Kaganda.

Mkurugenzi wa Halmshauri ya Mji wa Babati, Shaabani Mpendu amesema kuwa jumla ya Sh milioni 211 zimetolewa kwa vikundi mbalimbali ikiwa ni mikopo kwa ajili ya vijana, akina mama na makundi maalum na kwamba mkopo huo umetengwa kwa makundi matatu lakini kwa awamu ya kwanza hakuna kundi maalum.

Kwa kujibu wa Mpendu fedha hizo Sh milioni 211 tayari zimewekwa katika akaunti za vikundi ambavyo viliomba na kupata sifa pia zaidi ya Sh milioni 550 zimetengwa kwa ajili ya maombi mapya ya mkopo kwa vikundi vingine ikiwa ni mwendelezo wa jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea maendeleo wananchi.

Aidha amewataka wadaiwa sugu kurejesha fedha walizokopa siku za nyuma jumla ya Sh milioni 80 ambazo amesema halmashauri inaendelea na jitihada mbalimbali za kupata fedha hizo.