GEITA: JUMLA ya vikundi 39 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu sawa na asilimia 82 ya vikundi 47 vilivyoomba mkopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita vimepatiwa tangu kurejea wa mikopo hiyo.
Mkopo huo una jumla ya Sh milioni 689 ambapo vikundi 23 vya wanawake vimepatiwa sh milioni 351, vikundi 14 vya vijana vimepatiwa sh 239 na vikundi viwili vya watu wenye ulemavu vimepatiwa Sh milioni 45.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa halmashauri, Jonas Kilave ametoa taarifa hiyo katika hafla ya kukabidhi mkopo huo kwa wanufaika iliyofanyika Ofisi za Halmashauri zilizopo Kata ya Nzera.
“Vikundi nane havijakidhi vigezo kwa sababu mbalimbali ikiwemo kutofautiana kwa taarifa za kibenki na mfumo wa usajili, vimepewa maelekezo ya kurekebisha taarifa zao”, amesema Kilave.
Amesema tayari mafunzo kwa vikundi vilivyopatiwa mkopo yameletolewa yakihusisha watalaamu wa biashara, kilimo na ufugaji, kulingana na mahitaji ya miradi ya kikundi.
“Aidha wanakikundi wamepata mafunzo kuhusu utunzaji wa kumbukumbu za kikundi, usimamizi wa fedha, umuhimu wa akiba na kutatua migogoro”, amesema Kilave.
Amesema pia kiasi cha sh bilioni 1.2 kwa awamu ya pili ya utoaji wa mikopo kuanzia Januari hadi Machi, 2025 na tayari halmashauri imepokea maombi ya vikundi 58 kwa njia ya mtandao ambapo mwisho ni Februari 17, 2025.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Geita, Karia Rajabu amesema wameweka mpango maalum wa watalaamu kutembelea vikundi hivo mara kwa mara kutoa ushauri jinsi ya kujiendesha.
“Tutakapopita tuone jinsi gani manaorodhesha mapato manayoyapata, katika matumizi mnayotumia, hii itawajenga na hata wataalamu wataweza kuwashauri kwa uzuri zaidi”, amesema.
Mwenyekiti wa halmashauri, Charles Kazungu amesema Baraza la Madiwani litaendelea kusimamia kuhakikisha fedha inatengwa kwa jaili ya vikundi vya wajasiliamali wadogo kwa kila bajeti ya mwaka.
“Niwaombe sana nendeni mkazifanyie kazi mliokusudia, tunao uzoefu, vipo vikundi vikipata fedha cha kwanza ni kwenda kugawana fedha za matumizi, zingatieni malengo yenu”, amesema.
Katibu Tawala wa wilaya ya Geita, Lucy Beda amekemea migogoro kwa wanufaika wa mikopo hiyo kwani imekuwa kikwazo cha kufikia malengo na hata kukwamisha marejesho.
“Tuzingatie uwazi, kila mmoja awe na taarifa sahihi, kila mmoja awe anafahamu kwenye kikundi kitu gani kinaendelea, hii itatusaidia kutuweka pamoja na kuona kwamba wapi tunaelekea”, ameelekeza Beda.