Vilio vyatawala waliokufa ajalini Same wakiagwa

MAMIA ya watu wamejitokeza kuaga miili ya wanakwaya watano wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT) Usharika wa Wazo Hill, Dar es salaam waliokufa kutokana na ajali ya gari iliyotokea Same mkoani Kilimanjaro.

Vilio na manjozi vimetawala kwa familia,ndugu na jamaa  baada ya miili hiyo kuwasili kanisani kwa ajili ya ibada ya mwisho kabla ya kusafirishwa kwenda mikoa ya Kilimanjaro na Iringa maziko.

Miili hiyo imeagwa jana katika Kanisani la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Ushirika wa Wazo Hill dar es salaam.

Advertisement

Akizungumza katika Ibada hiyo, Askofu Mkuu, Dk Alex Malasusa amesema siku za kuishi duniani ni chache hivyo ni vyema kuwa na mpango mkakati wa maisha ya kiroho.

“Msiba huu utupe moyo wa hekima hasa katika suala la kumjua Mungu kwani siku za kuishi kwa mwanadamu ni chache sana,”amesema Dk Malasusa.

Dk Malasusa amesema watu hao ni washindi kwani waliishi vizuri na jamii hivyo liwe fundisho kwa wote wanaombaki kwa kutambua ni kitu ganijamii,familia au kanisa itajivunia siku haupo.

“Jeneza ni kibao cha kutukumbusha kuwa hata sisi safari yetu ni ileile ni wakati wa mimi na wewe kujiuliza siku tukiondoka duniani ni ni kitu gani kundi hili litajivunia.Siku hizi watu wanahubiri namna ya kupata mafanikio lakini wanasahau kuwa mafanikio hayo yanatoka kwa Mungu tena kwa imani na kuomba,”amesema .

Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani Goodluck Nkini amesema watawakumbuka wapendwa wao kwa kazi nzuri walioifanya enzi za uhai wao kwani kanisa lilijivunia uwepo wao na daima watakumbukwa.

Amesema majeruhi 13 waliokuwa wamesalia hospitali watano kati yao wameruhusiwa na waliobaki wamehamishiwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa ajili ya matibabu zaidi.

Ikumbukwe kuwa ajali hiyo ilitokea Oktoba 22 mwaka huu katika barabara ya Same mkoani Kilimanjaro wakati walipokuwa wakipeleka mwili wa mwanakwaya mwezao Machame Wilaya ya Hai Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi.

Waliofariki katika ajali hiyo ni Charles Mchome(63),Stephen Temba(39) wa jumuiya ya agape mwimbaji wa kwaya Kuu, mhudumu wa usharika na mwimbaji wa kwaya ya Uamsho,Neema Ngusi(37),Mtenzi wa jumuiya ya Tumaini na Mwimbaji wa kwaya ya wanawake Madelina Mwangika(61)na Katibu wa jumuiya ya Safina,Aurelia Soloka(54)