Viongozi wa dini wataka uchaguzi wa amani

DAR ES SALAAM – WAKATI nchi ikielekea kwenye Uchaguzi Mkuu 2025, Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), imetoa wito kwa vyama vya siasa, serikali na wananchi kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani, huru na haki na kuepuka siasa za uvunjifu wa amani.
Pia, imewataka Watanzania waache kuishia kulaumu serikali pale yanapotokea mapungufu badala yake wazungumzie pia mazuri na kujivunia maendeleo yanayoendelea kutekelezwa na serikali kwani pia ni dhambi kutozungumzia mazuri yaliyofanyika.
Hayo yalielezwa wakati wa Ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika kitaifa mkoani Morogoro katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Ifakara Mjini, Dayosisi ya Ulanga Kilombero.
Mwenyekiti wa CCT Mkoa wa Morogoro na Askofu wa KKKT Jimbo la Morogoro, Jacob Ole Mameo alikemea vitendo vinavyoligawa taifa akieleza kuwa mgawanyiko katika taifa huchochea kuleta maadui wa nje wasio na nia njema kwa taifa.
Alivitaka vyama vya siasa kutoingiza nchi katika migogoro isiyo na sababu akisisitiza matumizi ya 4R za Rais Samia Suluhu Hassan (Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga Upya) katika kufikia muafaka pale kunapotokea migongano.
“Kanisa linatoa wito kwa vyama vyetu vya siasa visituingize katika migogoro isiyo na sababu… Hatutaki mgawanyiko ndani ya taifa letu, hatutaki kumwagika damu,” alisema. Aliongeza: “Kifo cha Yesu Kristo na pazia kufunguka ni ushindi na upatanisho… ule usemi wa rais wa 4R utatuleta pamoja kujadili mambo yetu kama watu wenye akili na hekima,” alisema Askofu Poul.
Pia, aliwataka wale wanaohamasisha vurugu ndani ya taifa kuacha akisema taifa la Tanzania limepata uhuru bila vurugu hivyo nchi haiihitaji kumwaga damu ya kizazi cha sasa kwa sababu za kisiasa.
Aidha, alishauri uchaguzi huo uwe wa demokrasia kwa kuhakikisha Watanzania wanapata uhuru wa kutosha kuchagua viongozi wanaowataka katika hilo amewataka wanasiasa na wagombea kutangaza sera nzuri zitakazovutia wananchi na si kutoa rushwa.
“Demokrasia ni kuwapa watu uhuru wanaoutaka, vyama andaeni sera nzuri mzitangaze kwa wananchi ili sasa wao ndio wajue wanamchagua nani kutokana na sera yake,” alisisitiza.
Pia, Askofu huyo aliwataka wananchi kushukuru kwa maendeleo yanayofanywa nchini kwa kuwa serikali imejenga barabara, vituo vya afya na hata uwepo wa reli ya kisasa ya SGR.
“Taifa letu limefanya mambo mengi makubwa, wakati mwingine tunapenda kulaumu na kusahau yale mema yaliyofanyika, taifa limeleta mambo mengi ya mafanikio yaliyofanya tumeonekana tofauti na huko nyuma tunaona ujenzi wa barabara, afya, SGR … unaweza kukuta mtu kazi kulaumu tu hakuna shukrani,” alisema.
Askofu aliwataka pia watumishi wa serikali kama wasaidizi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa waadilifu kwa kutotoa taarifa za uongo kwa rais juu ya utekelezaji wa baadhi ya miradi. Aidha, aligusia suala la rushwa wakati wa uchaguzi kama moja ya changamoto katika uchaguzi mkuu na kulitaka taifa lirudi katika misingi ya haki.
“Rushwa inatajwa sana wakati wa uchaguzi na waumini wetu mnakula rushwa na hamtubu… wala rushwa hawatendi haki,” alisema. Kwa upande wa Katibu Mkuu wa CCT Taifa, Mchungaji Dk Canon Moses Matonya aliwakumbushia Wakristo kuombea uchaguzi mkuu uwe wa uhuru, haki na amani.



