Viongozi, wasomi wamlilia Ndugai

VIONGOZI akiwemo Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson wamemlilia Spika mstaafu na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kongwa, Job Ndugai ambaye amefariki dunia.

Katika ukurasa wake wa mtandano wa Instagram, Dk Tulia ameandika: “Dear Boss. Dear counselor, may the good Lord give you eternal peace, rest. Amen,” akimaanisha mpendwa bosi, mpendwa mshauri, mwenyezi Mungu akupe amani na pumziko la milele. Amina.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba kupitia ukurasa wake wa X alieleza kusikitishwa na taarifa za kifo cha Ndugai.

Naye aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde pia aliandika: “Pumzika kwa amani Job Yustino Ndugai, Spika mstaafu na Mwenyekiti wa Wabunge wa Mkoa wa Dodoma, Mwenyezi Mungu akupokee baba.”

Pia, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso aliandika kuwa: “Pumzika kwa amani mzee wetu Spika mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Kongwa.”

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Gerson Msigwa kupitia ukurasa wake aliandika: “Lala salama mjomba, poleni wana familia, ndugu jamaa na marafiki na wana Kongwa, daima tutakumbuka mchango wa mzee wetu Ndugai”.

Naye mdhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Paul Loisulie alisema Ndugai alikuwa ni mtu mwenye msimamo usioyumba katika kulinda na kutetea maslahi na rasilimali za nchi.

“Tangu akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Maliasili, na baadaye Mwenyekiti wa Bunge, Naibu Spika na kisha kuwa Spika wa Bunge, ukiachana na matukio machache ya upendeleo lakini kwenye kamati alizohuduma na hata alizoziunda alionesha kuwa ni mwenye msimamo wa kulinda na kutetea maslahi ya nchi na misimamo yake ilikuwa dhabiti kwenye hilo,” alieleza.

Alisema Ndugai pia alikuwa ni mwanasisa mwenye ushawishi na kukubalika na wengi na kwa urahisi.

“Alikuwa ni mwanasiasa mwenye uwezo wa kushawishi na kukubalika na wengi na ndio maana unaona katika miaka yote akiwa mbunge amepanda kidogo kidogo hadi kufikia kuwa kiongozi mkuu wa muhimuli huo,” alisema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button