Vipimo vya vinasaba vyatoa matumaini wanaopoteza ujauzito

DAR ES SALAAM: WANANDOA wanaopoteza mimba mara kwa mara licha ya kupata matibabu ya uzazi wanaweza kunufaika na uchunguzi wa vinasaba unaosaidia kubaini hitilafu za kromosomu katika viinitete, mojawapo ya sababu zinazoweza kuchangia mimba kuharibika katika hatua za awali za ujauzito.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wanasema uchunguzi huo si suluhisho la kila tatizo la uzazi, bali ni mojawapo ya njia zinazoweza kusaidia kuboresha uelewa wa sababu za baadhi ya mimba kuharibika na kuongoza maamuzi ya matibabu kwa wanandoa wanaokabiliwa na changamoto hiyo.

Uchunguzi huo unaojulikana kama Preimplantation Genetic Testing for Aneuploidy (PGT-A), hufanyika kwa viinitete vinavyotengenezwa kupitia teknolojia ya urutubishaji wa yai nje ya mwili (IVF), kabla ya kiinitete kuhamishiwa kwenye mfuko wa uzazi.

Kwa kutumia kipimo hicho, wataalamu huchunguza idadi ya kromosomu za kiinitete ili kubaini kama kuna hitilafu zinazoweza kuathiri ukuaji wake. Kromosomu hubeba taarifa za kinasaba zinazohitajika katika ukuaji wa binadamu.

Daktari wa Kituo cha Huduma za Uzazi cha Nu Life Fertility Centre, Sheila Ramadhani, alisema hitilafu za kromosomu ni miongoni mwa sababu zinazoweza kusababisha mimba kuharibika katika miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito.

Alisema baadhi ya wanandoa hupoteza mimba mara mbili au tatu, huku wengine wakishindwa kupata ujauzito licha ya kupitia matibabu mbalimbali ya uzazi, hali inayoweza kuhitaji uchunguzi zaidi ili kubaini sababu zinazochangia changamoto hizo.

Kwa mujibu wa wataalamu, kipimo cha PGT-A hufanyika baada ya mayai kurutubishwa na mbegu za kiume nje ya mwili na viinitete kufikia hatua maalumu ya ukuaji, kabla ya kufanyiwa uchunguzi wa vinasaba.

Mkurugenzi wa Tiba wa kituo hicho, Dk Madhav Hiran, alisema utaratibu huo unahusisha kuchukua sampuli ndogo ya seli kutoka kwenye tabaka la nje la kiinitete kilichofikia hatua ya blastocyst, kwa kawaida siku ya tano tangu kuanza kukua.

Alisema sampuli hizo hupelekwa maabara kwa uchunguzi wa kromosomu, hatua inayowasaidia wataalamu kutathmini viinitete kabla ya kufanya uamuzi kuhusu kiinitete kitakachohamishiwa kwenye mfuko wa uzazi.

Hata hivyo, PGT-A haiwezi kubaini kila aina ya tatizo la kinasaba wala kuhakikisha kuwa ujauzito utapatikana au mtoto atazaliwa akiwa hai. Uamuzi wa kutumia kipimo hicho unapaswa kuzingatia historia ya afya ya wanandoa, umri na tathmini ya wataalamu wa uzazi.

Kwa wanandoa wanaopoteza mimba mara kwa mara, wataalamu wanashauri kufanyiwa tathmini ya kitabibu ili kuchunguza sababu zinazoweza kuchangia hali hiyo, badala ya kudhani kuwa hitilafu za kromosomu ndizo chanzo pekee.

Uelewa wa sababu hizo unaweza kusaidia wanandoa kupata ushauri unaolingana na hali zao na kufanya maamuzi sahihi kuhusu hatua zinazofuata za matibabu ya uzazi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button