BAADA ya kukamilisha usambazaji wa umeme katika vijiji vyote 785 mkoani Mtwara, serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza mradi wa Sh bilioni 16.7 wa kusambaza umeme kwenye vitongoji 150 utakaonufaisha kaya 4,950 mkoani humo.
Mhandisi msimamizi wa wakala huo Kanda ya Kusini, Deogratius Nagu ametoa ufafanuzi huo Oktoba, 02, 2024 wilayani Masasi mkoani Mtwara mbele ya Mkuu wa Mkoa huo, Kanali Patrick Sawala wakati wa kumtambulisha mkandarasi atakayetekeleza mradi huo Kampuni ya Northern Engineering Works Ltd ya Arusha.
“Tunamshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kutuwezesha kukamilisha utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme kwenye vijiji vyote 785 mkoani hapa kwa asilimia 100 na sasa ni zamu ya vitongoji ambapo kiasi cha Sh bilioni 16.71 zitatumika kutekeleza mradi wa kusambaza umeme kwenye vitongoji 150,”amesema Nagu.
Tukio hilo lilishuhudiwa na viongozi wa Mkoa na Wilaya wakiwemo wakuu wa wilaya za Nanyumbu, Mtwara na Tandahimba, Kamati za Usalama Mkoa wa Mtwara na Wilaya ya Masasi, madiwani kutoka kata mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Masasi.
SOMA: REA wazindua mradi wa Sh Bil 11 Mtwara
Akizungumza wakati wa utambulisho wa mkandarasi huyo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala amewapongeza REA na Shirika la Umeme (TANESCO) kwa kuendelea kushirikiana kuhakikisha dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwaletea maendeleo wananchi wake kupitia nishati inatimia.
“Wana Mtwara tuna kila sababu ya kumshukuru Rais wetu mpendwa Dk Samia Suluhu Hassan na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko kwani kwa sasa hapa kila kijiji kina umeme na sasa wanahakikisha umeme unafika vitongojini,” amesema.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi wa kufikisha umeme vitongojini, Nagu amesema kati ya vitongoji 3,427 vilivyopo mkoani humo, vitongoji 2,200 vimefikishiwa umeme ambavyo ni sawa na asilimia 64 na kwamba vitongoji 150 ambavyo vitapata umeme kupitia mradi huo vitaongeza idadi ya vitongoji vyenye umeme katika Mkoa wa Mtwara.
SOMA: Vijiji vyote Mtwara kuwa na umeme
Amebainisha kuwa mradi huo ambao mkandarasi wake ametambulishwa, utatekelezwa kwa muda wa miezi 24 na hivyo kukamilika ifikapo Septemba 2026 na kuongeza kuwa vitongoji vitakavyobaki vitaendelea kupatiwa umeme kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mhandisi Nagu amesema mradi utatekelezwa katika majimbo 10 katika wilaya za Mtwara, Tandahimba, Newala, Masasi na Nanyumbu na kwamba katika kila jimbo vitongoji 15 vitanufaika.
“Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutuwezesha kukamilisha miradi ya kusambaza umeme kwenye vijiji vyote 785 Mkoani Mtwara; sasa ni zamu ya vitongoji; Tsh. bilioni 16.7 zitatumika kusambaza umeme kwenye vitongoji 150,” Mhandisi REA, Deogratius Nagu pic.twitter.com/Nbkwkoms88
— Wakala wa Nishati Vijijini (REA) (@WaNishati) October 2, 2024
“Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeendelea kutekeleza miradi mbalimbali katika Mkoa wa Mtwara ikiwa na lengo la kuwapatia huduma za Nishati wananchi ili kuboresha huduma za jamii maeneo ya vijijini na vijiji-miji,” amesema Nagu.
Kwa upande wake Mkandarasi aliyeshinda zabuni hiyo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Northern Engineering Works Ltd, Samwel Lema amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa mradi utatekelezwa kwa ubora unaotakiwa na utakamilika ndani ya muda kama ilivyo katika mkataba.