Vituo 73 vyasajiliwa huduma kuchuja damu

DODOMA; SERIKALI imesema hadi kufikia mwezi Machi 2025 jumla ya vituo 73 vimesajiliwa kutoa huduma ya kuchuja damu katika mikoa yote nchini kupitia hospitali za rufaa za mikoa, hospitali za rufaa za kanda, Hospitali Maalum, hospitali ya Taifa na hospitali binafsi.
Kauli hiyo imetolewa bungeni mjini Dodoma leo na Waziri wa Afya, Jenista Mhagama alipokuwa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2025/2026.
“Uwepo wa huduma za kuchuja damu karibu na wananchi kumeokoa maisha na kupunguza gharama za matibabu kwa wagonjwa wenye uhitaji.
“Aidha, Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imeendelea kuwekeza kwenye huduma za figo nchini kwa kuongeza mashine 137 za kuchuja damu katika hospitali 15 za umma na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vinavyotumika katika huduma za kuchuja damu kwa bei nafuu.
“Vilevile, Serikali imeendelea kuimarisha huduma za upandikizaji figo ambapo hadi kufikia mwezi Machi, 2025 jumla ya wagonjwa 155 walipatiwa huduma ya upandikizaji figo,” amesema Waziri Mhagama.