‘Vituo vya afya viheshimu wanufaika wa bima’

MKUU wa Mkoa wa Geita, Alexander Mnyeti amevitaka vituo vya kutolea huduma za afya vya umma na binafsi kuheshimu na kutoa huduma stahiki kwa wanufaika wa bima ya afya kwa wote.
Mnyeti ametoa maagizo hayo katika hafla ya uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Mpango wa Bima ya Afya kwa wote mkoani humo iliyofanyika katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro.
Amesema wanufaika wa bima ya afya kwa wote wanayo haki ya kupata huduma wanayostahili kwa mjibu wa mashariti ya bima na taratibu zilizowekwa na serikali na siyo vinginevyo.
“Hairuhusiwi mwananchi kunyimwa huduma kwa sababu zisizo halali, malalamiko yanayojitokeza yashughulikiwe kwa haraka na weledi”, amesema Mnyeti.

Aidha ameitaka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa kufuatilia malalamiko kadhaa yanayodai vituo vya kutolea huduma za afya vinatoa kipaumbele kwa wenye fedha taslimu na kupuuza wenye bima.
“Niwaombe sana watoa huduma siyo anapewa kipaumbele anayelipa fedha taslimu na mwenye bima ya afya anapuuzwa kwa sababu hatoi fedha taslimu”, amesema Mnyeti.
Mnyeti ameagiza wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na watendaji kuhakikisha wananchi wanapata elimu kuhusu umuhimu, faida, gharama na taratibu za kujiunga na bima.
Ameelekeza kila halmasahuri ifuatilie, kufanya tathimini na kuwasilisha taarifa kwa wakati baada ya siku 14 ili kubaini mafanikio, changamoto na hatua za kuboresha utekelezaji.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dk Omari Sukari amesema mkoa una watoa huduma za afya takribani 5,000 ambao watasaidia kutoa huduma kwa kila mtu ikiwemo wanufaika wa bima.

Amesema tayari mkoa umekamilisha kufunga mifumo ya kielektroniki inayosomana na mfumo wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuongeza ufanisi wa mpango wa bima ya afya kwa wote.
Meneja wa NHIF mkoa wa Geita, Sophia Kaku amesema katika awamu ya pili ya Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote mkoa umelenga kusajili kaya 26,377 zenye jumla ya wanufaika 93,157.



