Bei ya mafuta yazua ghasia Angola

LUANDA, ANGOLA : TAKRIBAN watu 22, wakiwemo raia na afisa wa polisi, wamefariki dunia huku wengine zaidi ya 200 wakijeruhiwa katika maandamano makubwa ya kupinga ongezeko la bei ya mafuta nchini Angola.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Manuel Homem, amesema maandamano hayo yaliyoanza Jumatatu wiki hii yamekuwa ya vurugu kubwa, yakihusisha wimbi la hasira ya umma lililochochewa na mgomo wa madereva wa teksi, kabla ya kuenea nchi nzima.

Polisi wamesema watu zaidi ya 1,200 wametiwa mbaroni katika operesheni zinazoendelea kudhibiti hali ya usalama, huku biashara na maduka makubwa yakiwa yamefungwa katika maeneo mbalimbali. Katika Jiji Kuu la Luanda, madaktari katika hospitali za umma wamesema huduma za dharura zimezidiwa uwezo ndani ya saa 24 zilizopita.
“Tumepokea waandamanaji wengi wakiwa na majeraha mabaya. Cha kusikitisha ni kwamba baadhi yao walifariki dunia. Tuna wasiwasi idadi ya vifo inaweza kuwa juu zaidi ya takwimu rasmi,” alisema daktari mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
Milio ya risasi imeripotiwa katika maeneo kadhaa ya jiji hilo tangu Jumatatu hadi Jumanne, hali iliyoongeza taharuki miongoni mwa wananchi, ambapo wengi wameamua kubaki majumbani. SOMA: Watu 108 wauawa kwa kipindupindu Angola



