Vyakula vyenye sukari, uchafu sababu watoto kutoboka meno

MATATIZO ya kutoboka kwa meno ni makubwa miongoni mwa watoto, sababu kubwa ni kutokana na tabia za kula vyakula vyenye sukari nyingi kama pipi na soda bila kutunza usafi wa kinywa.
Akizungumzia tatizo la kutoboka kwa meno jijini hapa, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Kinywa na Meno kutoka Hospitali Rufaa ya Benjamin Mkapa (BMH), Dk Alex Kimambo alisema tatizo ni kubwa hapa nchini ambapo linaathiri hasa watoto na vijana.
“Hali hiyo inazidi kuwa mbaya kwa watoto ambao mara nyingi hawapigi mswaki meno yao vizuri au mara kwa mara,” alisema.
Akizungumzia suala la elimu, alisema elimu kuhusu afya ya kinywa na meno bado haijafika kwa undani katika maeneo mengi nchini, hasa vijijini.
“Watu wengi hawajui jinsi ya kutunza afya ya kinywa na meno, kama vile umuhimu wa kupiga mswaki mara mbili kwa siku, kula vyakula bora, na kutembelea daktari wa meno mara kwa mara,” alisema.
Daktari huyo amesema huduma za afya ya meno ingawa zinapatikana katika miji mikubwa kama Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Mwanza, huduma hizo bado ni chache na hazipatikani kwa urahisi maeneo ya vijijini na pembezoni.
“Hali hii hufanya watu wengi kukosa huduma za uchunguzi na matibabu ya meno,” alisema.
Alisema udaktari wa kinywa na meno ni taaluma inayohitajika nchini na kwamba kuna uhaba wa wataalamu hao, hasa katika maeneo ya vijijini.
Dk Kimambo alisema hiyo ni changamoto kubwa kwa kuhakikisha kuwa watu wanapata huduma bora.
Akizungumzia juhudi za serikali na mashirika alisema serikali kupitia Wizara ya Afya, imekuwa ikifanya juhudi za kuongeza ufanisi katika huduma za afya ya kinywa na meno hiyo ni pamoja na kuanzisha kampeni za kuhamasisha usafi wa kinywa, kutoa huduma za bure au za gharama nafuu kwenye vituo vya afya.



