Vyama tawala Tanzania, Burundi vyasifu ujenzi SGR

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa Kigoma kimesema uwekaji jiwe la msingi kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Msongati Mkoa wa Burungu nchini Burundi hadi Uvinza ni mafanikio makubwa kwa chama hicho katika utekelezaji wa ilani yake ya uchaguzi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa Kigoma, Jamal Tamim akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwekwa jiwe la msingi la mradi huo katika hafla iliyoongozwa na Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan alisema kuwa utekelezaji wa ilani umefanya kazi kwa vitendo.
Tamim alisema kukamilika kwa mradi huo kuna manufaa makubwa kiuchumi kwa serikali za nchi hizo mbili, lakini zaidi manufaa hayo yanagusa moja kwa moja uchumi wa wananchi wa nchi hizo katika kufanya shughuli za biashara na uchumi.
“Tanzania na Burundi zina historia ya muda mrefu ya udugu wa damu, mfano ukiwemo wa wakimbizi wa Burundi ambao wanahifadhiwa Tanzania kwa miaka mingi, usuluhishi wa mgogoro wa Burundi na sasa ushirikiano katika utekelezaji wa mradi huu ambalo ni jambo kubwa katika kukuza diplomasia ya uchumi lakini pia ni ushirikiano wa kisiasa baina ya nchi hizo,” alisema.
Akizungumza, Bizimana Filemon kiongozi wa Chama cha CNDD-FDD Mkoa Burungu, alisema uwepo wa reli hiyo utarahisisha usafiri wa haraka wa abiria na mizigo kutoka nchini humo kwenda Tanzania hadi Bandari ya Dar es Salaam ambayo ni kiungo muhimu katika maendeleo ya kiuchumi ya nchi hiyo na kwamba uchumi wa Burundi kwa kupitia mradi huo utakuwa kwa haraka.
Majaliwa alisema kuwa mradi huo utachochea ukuaji wa uchumi kwa nchi hizo mbili, kuchochea ukuaji wa uchumi wa kikanda kwa nchi za Afrika Mashariki ambapo utakuwa kichocheo kikubwa katika ukuaji wa sekta ya biashara, kilimo, viwanda na madini.