‘Vyama viwape kipaumbele wenye ulemavu’

WADAU mbalimbali wa demokrasia wanakiri kuwa, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) mwaka huu imefanya juhudi kubwa kushirikisha watu wenye ulemavu katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2025.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na INEC, Daftari la Kudumu la Wapigakura linaonesha lina watu wenye ulemavu 49,000.

Ushirikishwaji huo wa INEC umelifurahisha kundi hilo, lakini linasema changamoto ipo katika namna ya kufikia mikutano ya kampeni na mazingira ya ukaaji na kusikiliza sera, ilani na ahadi za vyama na wagombea bila kuathiri na bughudha zinazotokana na msongamano wa watu.

SOMA: Wenye ulemavu watakiwa kupiga kura

Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu Tanzania (CHAWATA), Hamad Komboza anakiri kuwa, INEC imeshirikisha kwa kiasi kikubwa kundi hilo katika mchakato huo wa Uchaguzi Mkuu 2025. Anasema INEC imeshirikisha kundi hilo baada ya kuona umuhimu wa kuwashirikisha katika hatua zote za uchaguzi hadi kupata matokeo ya uchaguzi bila kuwatenga watu wenye ulemavu.

“Kama tume ilivyofanya katika mchakato wote kwa kutushirikisha nao wagombea wanatakiwa wafahamu kuwa kundi hili lina umuhimu mkubwa na linapaswa kupewa kipaumbele hasa wakati huu nchi inavyoendelea na kampeni,” anasema.

Anaongeza: “Kama tume ilivyofanya katika mchakato wote kwa kutushirikisha nao wagombea wanatakiwa wafahamu kuwa kundi hili lina umuhimu mkubwa na linapaswa kupewa kipaumbele hasa wakati huu nchi inavyoendelea na kampeni,” anasema.

Anasema: “Vyama viwape kipaumbele wenye ulemavu… Kinachotakiwa katika kipindi hiki ni wagombea kukumbuka kutenga maeneo ya kukaa watu wenye ulemavu pembezoni mwa majukwaa wanayotumia kunadi sera katika kampeni zinazoendele nchi nzima.”

Anaongeza: “Baada ya kampeni kinachofuatia ni upigaji kura; watu wenye ulemavu tunatakiwa tupate nafasi nzuri na salama kusikiliza sera za vyama vinavyoshiriki kwenye uchaguzi ili hatimaye na sisi tufanye maamuzi sahihi wakati wa kupigakura kwa kuchagua chama tunachoona sera zake zitakuwa ni mtetezi wetu.”

Anasema ingawa vyama vimeanza na vinaendelea na kampeni katika maeneo mbalimbali nchini, hadi sasa havijaweka mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu kufika na kusikiliza sera za vyama kwa usalama zaidi bila kuathirika na msongamano wa watu.

“Bado tunaona hakuna ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu kikamilifu ili waweze kwenda maeneo ambayo vyama vinanadi sera zao na kupata nafasi nzuri kuwasikiliza,” anasema. Komboza anaongeza: “Kwa kweli vyama vinapaswa kutupa kipaumbele sisi watu wenye ulemavu kwa sababu hili ni kundi kubwa lenye wapigakura zaidi ya 49,000…”

Kwa mujibu wa Chawata, vyama vya siasa katika kampeni havina budi kuhakikisha watu wenye ulemavu wanaondolewa vikwazo vya kushiriki kikamilifu katika kampeni kwa sababu ni haki yao ya msingi kama ilivyo kwa wengine ili wasilikilize na kuzijua sera za vyama na wagombea kabla ya kwenda kuwapigia kura.

Anashauri vyama vya siasa kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya kukaa watu wenye ulemavu katika viwanja walivyoandaa kufanyia mikutano ya kampeni. Anasema hali hiyo itawezesha kundi hilo kusikiliza kwa umakini sera za wagombea.

“Vyama viangalie au vijiulize vinatoa mazingira gani mahsusi kwa ajili yetu sisi watu wenye ulemavu… Katika hii mikutano ya kampeni vyama vya siasa visituchukulie kijumlajumla kama watu wasio na ulemavu hii si sawasawa,” anasema.

Katika mkutano wa kampeni wa chama kimoja (jina tunahifadhi) mkoani Dar es Salaam, akiwa kando kabisa ya uwanja, mwanamke mke mmoja mwenye ulemevu wa viungo anasikika akisema: “Hapa panatosha ingawa sioni wala kusikia vizuri yanayosemwa maana hizo harakati hizo siziwezi.”

“Vyama vinatamani hata sisi watu wenye ulemavu tufike kwenye kampeni zao, lakini hatuwezi kufika kwa sababu mazingira yetu ni magumu lakini pia tunapata hofu ya kwenda kushiriki kwa sababu mazingira ya maeneo yanakuwa si rafiki kwetu na yanakuwa kizuizi kikubwa kwetu,” anasema Komboza.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Said Msonga anasema mazingira bora kwa watu wenye ulemavu wakati wa kampeni yalipaswa kuhimizwa tangu hatua za awali kuanzia INEC kwa kutengeneza mazingira ya kipekee kwa watu hao.

Kwa mujibu wa Msonga, hata wadau wa uchaguzi wanaoshiriki nao walitakiwa kupanga utaratibu na kutenga wakati maalumu ili kulisaidia kundi hilo.

“Hili ni kundi ambalo huko nyuma lilikuwa linaachwa mbali zaidi pengine kwa kutoshirikishwa, lakini wenyewe walikuwa wanajitahidi kuhamasishana na kutengeneza mwamko wa kushiriki ili kutumia haki yao ya kikatiba,” anasema Msonga.

Anaongeza: “Katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2019, wagombea takribani 3,000 walishinda lakini hawa zaidi ya 3,000 wanatokea kwenye kundi la watu wenye ulemavu.” “Unaweza kuona ni kwa kiasi gani mwamko wa kundi la watu wenye ulemavu umekuwa mkubwa katika kuendea siasa na kushiriki uchaguzi; kuchagua na kuchaguliwa,” anaeleza.

“Nimeangalia na kufuatilia katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 chama cha MAKINI kilitoa tangazo kikisisitiza kuwa, watu wenye ulemavu wanaweza kuchukua fomu za chama hicho kuwania nafasi za uongozi bila kulipia gharama na hili ni tofauti na vyama vingine vyote.”

Anasema linapokuja suala nyeti kama la uchaguzi kwa nafasi mbalimbali, watu wenye ulemavu wanapaswa kupewa kipaumbele na umuhimu wa kipekee katika mchakato wote na kwa wadau wote.

“Chama cha MAKINI angalau wameweza kutilia maanani walemavu na pia tumekuwa tukishuhudia hivyo hata katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), lakini katika idadi ya vyama vilivyopo, vinavyotoa kipaumbele kwa wenye ulemavu ni vichache,” anasema Msonga.

Kwa mujibu wa Msonga, ingawa sheria na kanuni zinazotumika katika mchakato wa uchaguzi zinatoa haki sawa kwa watu wenye ulemavu kuchagua na kuchaguliwa, bado nafasi yao haipewi uzito unaostahili. Anasema idadi ya watu 49,000 wenye ulemavu waliojiandikisha katika daftari la wapigakura kufanya jimbo la uchaguzi kwa kuwa inatosha kumuingiza mtu bungeni.

“Kwa hiyo ilipaswa idadi hii ipewe nafasi na umuhimu wa kipekee… Japo tunafahamu hata INEC katika mazoezi ya kujiandikisha inajitahidi kuwapa elimu na kipaumbele cha kupiga kura wanapofika kwenye vituo vya kupigia kura,” anasema.

Msonga anaongeza: “Ni muhimu vyama vya siasa vinavyoendelea na kampeni kutenga maeneo kwa ajili ya watu wenye ulemavu kwa sababu kuna wengine wanaweza kuwa wanahofia kwenda kutokana na hii mijumuiko na wanaogopa kuchangamana na watu wengine ili kuepuka madhara.”

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button