Wenye ulemavu watakiwa kupiga kura

MBUNGE wa Viti Maalum anayewakilisha watu wenye ulemavu Tanzania, Stella Ikupa amewataka watu wenye ulemavu kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, mwaka huu.

Akizungumza katika vituo vya watu wenye ulemavu, wasafirishaji abiria kupitia bajaji ndogo na kubwa, jijini Dar es Salaam mbunge huyo amewapongeza wasafirishaji hao wenye ulemavu  kwa kuendelea kuiunga mkono kupitia kuisemea vizuri kwa kazi kubwa zinazotekelezwa na serikali.

Advertisement

Amewasisitiza wasafirishaji hao kuendelea kuiunga mkono serikali kwa kujitokeza kupigia kura viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Vituo alivyotembelea Ikupa ni  Nyahaja Uhasibu Group kilichopo pembezoni mwa Chuo Cha Uhasibu (TIA), Temeke, Kituo cha Ocean Road cha bajaji ndogo cha wanawake, kituo cha bajaji kubwa na ndogo cha feri cha wanaume,(UWABADA) kituo cha wanaume cha Mnazi Mmoja (UWABAKUTA)

“Lengo la kuwafikia siku ya leo ni kuwahamasisha na kuwakumbusha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ulioko mbele yetu, unaotarajiwa kufanyika Jumatano Novemba 27, kwani ni haki ya kila mwananchi kumchagua kiongozi anayemtaka,”amesema.