Vyombo vya habari mbioni kupata ruzuku

SERIKALI imesema inatafakati kuona namna ya kufadhili vyombo vya habari kwa kuvipa ruzuku.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema vyombo vya habari ni sehemu muhimu katika jamii yoyote iliyostaarabika.

Profesa Kitila alisema hayo Dar es Salaam alipozungumza na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na waandishi wa habari jana.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) inatambua na kuthamini mchango wa vyombo vya habari katika kukuza uwajibikaji na kuimarisha utawala bora nchini.

Profesa Kitila alisema dhamira ya serikali ya kuimarisha vyombo vya habari kwa kutoa ruzuku zitakazotokana na kodi za wananchi bila kuathiri uhuru wa habari.

“Tumeweka haja ya kuendelea kuimarisha vyombo vya habari, tunatafakari namna gani ambayo vyombo vya habari vinaweza kufadhiliwa kupitia kodi za Watanzania kwa sababu haiwezekani mkawa na vyombo vya habari ambavyo hamjui vyanzo vyake vya fedha, vya kubahatisha,” alisema.

Profesa Kitila alisema lengo la serikali ni kuviwezesha vyombo vya habari kufanya kazi yake kwa ukweli, uwazi na kwa kuzingatia taaluma ya uandishi wa habari na si kuviimarisha viwe vinapendelea.

Alisema mchakato wa katiba mpya hauwezi kuathiri utekelezaji wa Dira 2050 kwa kuwa moja ya kipengele katika dira hiyo ni utawala bora.

“Dira yenyewe imetambua kwenye moja ya eneo la utawala bora ikisisitiza kuwa na katiba imara na ikaongeza kuwa katiba imara inayotokana na mwafaka wa kitaifa,” alisema Profesa Kitila.

Pia, alisema katika kuimarisha sekta ya afya kupitia Dira 2050, wameweka mikakati ya kuzingatia afya kwa Watanzania akisisitiza kuwa watakusanya vyanzo kwa ajili ya mfuko wa bima ya afya kusaidia Watanzania.Profesa Mkumbo alisema rais atakayeingia madarakani atatakiwa kuizingatia dira hiyo kwa kuwa mipango ya mambo yanayotarajiwa kufanyika yapo katika dira hiyo.

Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile alihimiza ilani za vyama vya siasa vyenye kushiriki uchaguzi mkuu ziakisi malengo na mipango iliyopo kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025-2050.

“Dira hii si kwa ajili ya Chama Cha Mapinduzi pekee maana baadhi ya watu wanaweza wakachanganya kuwa hii dira ni ya CCM, vyama vyote vya siasa vinavyoenda kuandika ilani zao vinapaswa kuakisi dira hii na wakifanya hivyo sisi hatutasita kuandika habari zao,” alisema Balile.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button