Waagizwa kuzingatia usalama mahali pa kazi

MKUU wa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Remidius Emmanuel amewataka wafanyakazi wa kampuni ya ujenzi ya GS Contractors kuzingatia tahadhari za afya na usalama mahali pa kazi ili kukuza tija kupitia utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

Alitoa agizo hilo Jumamosi alipofanya mazungumzo na wafanyakazi wa kampuni hiyo wakati akikagua ujenzi wa daraja la Makawa lenye urefu wa meta 31.9 linalounganisha Kijiji cha Makawa na Mageseni.

Wafanyakazi hao walisema kwa sasa hawana mgogoro na mkandarasi isipokuwa wanakabiliwa na upungufu wa vifaa vya usalama mahali pa kazi ikiwemo maski na kofia ngumu, hali inayowaweka kwenye mazingira hatarishi.

Kutokana na changamoto hiyo, Mkuu wa Wilaya aliwashauri wafanyakazi wa kampuni hiyo kuchukua tahadhari kwa kutunza usalama wa afya zao wakati wa utekelezaji mradi na hivyo kutoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) Wilaya ya Kongwa, Peter Johnson kuhakikisha mazingira yanakuwa rafiki kwa afya za wafanyakazi hao.

Mradi huo wenye thamani ya Sh milioni 598 unatekelezwa na Kampuni ya GS Contractors na kusimamiwa na Tarura Wilaya ya Kongwa. Utakapokamilika utaunganisha wakazi wa vijiji vya Makawa na Mageseni ambao wamekuwa wakikabiliwa na adha ya usafiri kwa muda mrefu.

 

 

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button