PAMOJA na kutokuwa na malengo yoyote ya kisiasa wala ya kibiashara, Jumuiya ya Waislamu Waahmadiyya inawataka waumini wake kuwa raia wema na watiifu kwa serikali iliyopo madarakani.
Amiri na Mbashiri Mkuu wa Jumuiya hiyo nchini, Khawaja Muzaffar Ahmad, amewahimiza waumini wa dini hiyo kudumisha amani, kuwapenda watu wote, na kujitolea kwa maendeleo ya taifa lao.
Katika ziara yake ya siku tatu mkoani Iringa, Amiri huyo alisisitiza kuwa Uislamu siyo dini ya vurugu, bali ya amani na ustawi wa kijamii.
“Kupitia misingi ya dini hii, tunafundishwa kuishi kwa amani, upendo, kuheshimiana, na kuvumiliana na watu wa dini nyingine pamoja na jamii nzima. Tumekuwa tukifanya mikutano ya amani katika mikoa mingi nchini ili kueneza ujumbe huu,” alisema Ahmad.
Mbashiri Mkuu alitoa wito kwa jamii kuweka mkazo kwenye malezi bora na maadili kwa watoto ili kujenga kizazi chenye ustawi na kuzingatia heshima na maadili ya dini.
Alisema kuwa malezi ya vijana ndiyo msingi wa kuunda jamii yenye kumcha Mungu, na yenye uwezo wa kupambana na kuondoa ukatili, mmomonyoko wa maadili kama ubakaji, ulawiti, na tabia zisizoendana na maadili mema.
Akizungumza kuhusu masuala ya maendeleo, ajira, na ujasiriamali kwa waumini wao, Ahmad aliwahimiza vijana kujituma katika elimu na kupata ujuzi ambao utawasaidia kupambana na changamoto za kiuchumi na hivyo kuondokana na umasikini.
“Elimu ni ufunguo wa maisha. Watanzania na waumini wetu wakiwekeza kwenye elimu, hiyo ni njia bora zaidi ya kukabiliana na changamoto za maendeleo kwa ujumla,” alisema.
Ziara hii ya Amiri wa Jumuiya ya Waislamu Waahmadiyya imepokelewa kwa furaha na viongozi wa dini, wananchi, na wanachama wa jumuiya hiyo, ambao wanatarajia mwendelezo wa shughuli zinazolenga kuleta amani na mshikamano katika jamii.
Mwisho wa ziara yake, alifanya maombi ya pamoja ya amani kwa taifa huku akihimiza umuhimu wa mshikamano na maadili mema miongoni mwa Watanzania.