Waajiri wapewa neno fedha za waajiriwa

MTWARA: WAAJIRI wametakiwa kutambua kuwa, kukata fedha za waajiriwa wao kwa ajili ya kuwasilisha michango kwenye Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kushindwa kuziwasilisha ni kosa la uhujumu uchumi kwa mujibu wa sheria.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Mtwara Richard Mwalingo wakati wa jukwaa la pamoja kati ya NSSF na waajiri lililofanyika katika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara.
“Kitendo hicho kinachofanywa na baadhi ya waajiri kinahesabika kama matumizi mabaya ya ofisi jambo ambalo linaweza kusababisha mwajiri kushtakiwa kwa kosa la uhujumu uchumi”amesema Mwalingo
Aidha amewataka waajiri hao kufuata matakwa ya kisheria yaliyoainishwa kwa mujibu wa sheria pia waache kutoa taarifa za uongo au kuingia kwenye mtego wa kumkata mwajiriwa michango kisha kumpa fedha hizo mkononi badala ya kuziwasilisha kwenye mfuko husika.

“Siku mwajiriwa akiachishwa kazi au akaacha kazi na kuja na mkataba wake sisi kama serikali hatutahangaika na mfanyakazi tutamuuliza mwajiri hii michango iko wapi? kwa sababu sheria imemuelekeza mwajiri na si mfanyakazi”amesisitiza Mwalingo
Nae Meneja wa NSSF Mkoa wa Mtwara, Rebure Maira alisema hadi sasa jumla ya Sh bilioni 3.7 bado hazijalipwa na zipo kwa waajiri ambapo tatizo kubwa likiwa kwa waajiri wanaokata michango ya wafanyakazi hawawasilishi kwenye mfuko hali inayomfanya mwanachama kuamini kuwa fedha zake zipo NSSF.
Amesema miongoni mwa hatua wanazochukua ili kuhakikisha waajiri wanalipa kwa wakati ikiwamo kutoa elimu ya kuwakumbusha wajibu wao wa kisheria huku wakibaini kuwepo kwa pengo kubwa la waajiri kushindwa kulipa michango kwa wakati.
Aidha, ametoa wito kwa waajiri hao kutoisubiri nguvu ya mahakama bali wawajibike kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwenye mfuko ili waweze kulipwa mafao yao kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili.



