Waandishi watano Al Jazeera wauawa Gaza

GAZA, PALESTINA : KITUO cha Habari cha Al Jazeera kimethibitisha waandishi wake watano kuuawa katika shambulio la anga la Israel lililotokea karibu na lango kuu la Hospitali ya Al-Shifa, mjini Gaza.
Taarifa ya kituo hicho iliwataja waandishi waliouawa kuwa ni Anas al-Sharif na Mohammed Qreiqeh, pamoja na wapiga picha Ibrahim Zaher, Mohammed Noufal na Moamen Aliwa ambao wote walikuwa ndani ya hema maalumu la waandishi wa habari lililokuwa hospitalini hapo wakati walipolengwa moja kwa moja na shambulio hilo.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limekiri kutokea kwa shambulio hilo na kudai kuwa shambulio hilo lilimlenga Anas al-Sharif kwa madai kuwa alikuwa kiongozi wa kikosi cha wapiganaji wa Hamas. SOMA: Mashambulizi ya Israel yanateketeza familia Gaza
Mhariri Mkuu wa Al Jazeera, Mohamed Moawad, aliliambia BBC kuwa al-Sharif alikuwa mwandishi aliyeidhinishwa rasmi na ndiye mtangazaji pekee wa kituo hicho ndani ya Ukanda wa Gaza. Moawad aliongeza kuwa tangu kuanza kwa vita, Israel haijaruhusu waandishi wa kimataifa kuingia Gaza, hivyo vyombo vingi vya habari duniani vimekuwa vikiwategemea waandishi wa eneo hilo.
“Walilengwa wakiwa kwenye hema lao, hawakuwa mstari wa mbele wa mapigano,” alisema Moawad, akiongeza kuwa hatua hiyo inalenga kuwanyamazisha waandishi kuripoti taarifa kutoka Gaza.
Kwa mujibu wa taarifa, dakika chache kabla ya kuuawa, al-Sharif, mwenye umri wa miaka 28, alichapisha ujumbe kwenye mtandao wa X akielezea mashambulizi makali ya mabomu mjini Gaza. Chapisho lingine lililofuata, ambalo linaaminika kuandaliwa mapema, lilichapishwa na rafiki yake baada ya kifo chake.
Video zilizothibitishwa na idara ya uhakiki ya BBC zilionyesha watu wakibeba miili ya waandishi waliouawa, huku majina ya Qreiqeh na al-Sharif yakitajwa kwa uchungu na mashuhuda waliokuwa na nembo za “vyombo vya habari”.
IDF ilimshutumu al-Sharif kwa kujifanya mwandishi wa habari, ikidai kuwa alikuwa mhusika mkuu katika kupanga mashambulizi ya roketi dhidi ya raia na wanajeshi wa Israel, na kudai ilishapata taarifa za kijasusi kuhusu ushiriki wake kwenye mafunzo ya kijeshi. Mwezi mmoja kabla ya mauaji hayo, Al Jazeera, Umoja wa Mataifa na Kamati ya Kuwalinda Waandishi wa Habari (CPJ) walitoa taarifa wakionya kuwa maisha ya al-Sharif yako hatarini na kutoa wito wa kulindwa kwake.
Mkurugenzi Mtendaji wa CPJ, Jodie Ginsberg, aliliambia BBC kuwa Israel imeshindwa kuwasilisha ushahidi wa kuthibitisha madai kwamba waandishi waliouawa walihusiana na ugaidi. “Huu ni mwenendo wa muda mrefu ambapo mwandishi huuawa na baadaye Israel hudai alikuwa gaidi bila ushahidi wa kutosha,” alisema.
Tukio hili linafuatia matukio mengine ya waandishi wa Al Jazeera kuuawa Gaza. Mwaka jana, Ismael Al-Ghoul aliuawa katika shambulio la anga akiwa ndani ya gari lake, tukio lililosababisha pia kifo cha mpiga picha Rami al-Rifi na kijana mmoja aliyekuwa akipita kwa baiskeli.
Kwa mujibu wa CPJ, waandishi wa habari 186 wamethibitishwa kuuawa tangu kuanza kwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 2023.



