Wabakaji Madagascar kuhasiwa

BUNGE la Madagascar limepitisha sheria inayoruhusu kuhasiwa kwa upasuaji kwa watakaopatikana na hatia ya ubakaji wa watoto.

Sheria hiyo imesababisha ukosoaji kutoka kwa mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu, lakini pia imepata kuungwa mkono na wanaharakati ambao wanasema ni kizuizi mwafaka kwa ubakaji.

Bunge nchini humo lilipitisha sheria hiyo mnamo Februari 2 na Seneti, baraza la juu, liliidhinisha wiki iliyopita.

Ni lazima sasa iidhinishwe na Mahakama Kuu ya Kikatiba na kutiwa saini kuwa sheria na Rais Andry Rajoelina, ambaye alizungumzia suala hilo kwa mara ya kwanza mwezi Desemba.

Waziri wa Sheria Landy Mbolatiana Randriamanantenasoa alisema ni hatua ya lazima kwa sababu ya ongezeko la kesi za ubakaji wa watoto.

Wahalifu pia wangekabiliwa na vifungo vikali vya hadi maisha jela pamoja na kuhasiwa.

Habari Zifananazo

Back to top button