Wabunge 47, naibu mawaziri wanane chali!

DAR ES SALAAM; NAIBU Mawaziri wanane na wabunge waliomaliza muda wao wapatao 47 wameshindwa kuchomoza katika kura za maoni za kuomba kugombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Matokeo ya uchaguzi huo yaliyotolewa kutoka mikoa mbalimbali yanaonesha naibu mawaziri hao katika Serikali ya Awamu ya Sita ni pamoja na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo (Maswa Mashariki), Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe (Mufindi Kaskazini) na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Danstan Kitandula (Mkinga).

Wengine ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geofrey Pinda (Kavuu), Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti (Misungwi) na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini (Butiama).

Wengine ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Chilo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi (Mafinga Mjini).

Kwa upande wa Zanzibar, naibu mawaziri watatu wameshindwa katika kura za maoni akiwemo Naibu Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi, Nadir Abdulatif Al-Wardy, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Juma Makungu.

Katika uchaguzi huo ambao wabunge wakongwe wanawake wameng’ara majimboni, miongoni mwao wamo wawili waliohamia CCM hivi karibuni kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambao ni Kunti Majala (Chemba) na Jesca Kishoa (Iramba Mashariki).

Lucy Mayenga ameongoza Jimbo la Kishapu kwa kura 7,814 kati ya kura halali 12,864.

Munde Tambwe ameongoza Jimbo la Sikonge mkoani Tabora kwa kura 5,296 akifuatiwa na Amos Maganga (695), Said Lyoba (597), Joseph Kakunda (504), Samwel Chitalilo (437) na Nyaso Gama (8).

Rita Kabati ameongoza Jimbo la Kilolo kwa kupata kura 4,565 akifuatiwa na Novat Mfalamagoha aliyepata kura 3,845.

Miongoni mwa wakongwe walioshindwa kuongoza kwenye kura hizo ni waliokuwa wabunge wa viti maalumu kupitia Chadema, Ester Bulaya (Bunda Mjini), Ester Matiko (Tarime Mjini), Sophia Mwakagenda (Rungwe) na Nusrat Hanje (Ikungi Mashariki).

Katavi

Katika Jimbo la Kavuu, Aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi, Geophrey Pinda ameshika nafasi ya tatu kwa kura 969 baada ya Laurent Luswetula kupata kura 1,564 akifuatiwa na Prudenciana Kikwembe 1,065 na Dama Lusangija kura 901.

Mafinga Mjini

Dickson Lutevele ameongoza Mafinga Mjini kwa kura 1,219 akifuatiwa na Agrey Tonga (878) na Cosato Chumi (376).

Geita

Aliyekuwa mbunge wa Geita Mjini, Costantine Kanyasu, aliyekuwa mbunge wa Busanda, Tumaini Magesa na aliyekuwa mbunge wa Chato, Dk Medard Kalemani wameshindwa kwenye kura za maoni.

Kanyasu ameshika nafasi ya pili kwa kura 2,097 nyuma ya mshindani wake, Chacha Wambura aliyeongoza kwa kura 2,145.

Magesa ameshika nafasi ya tatu katika Jimbo jipya la Katoro kwa kupata kura 1,265 huku Kija Ntemi akiwa na kura 2,134.

Dk Kalemani wa Chato Kaskazini ameshika nafasi ya pili kwa kura 1,390 nyuma ya aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Geita, Cornel Magembe (4,298).

Katika Jimbo la Nyang’hwale, mbunge aliyemaliza muda wake, Hussein Nassoro ameongoza kwa kkura 3,875 na aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Geita, Joseph Msukuma amepata kura 5,251.

 Mara

Katika Jimbo la Tarime, Matiko amepata kura 196 wakati aliyekuwa mbunge wa Tarime Mjini, Michael Kembaki ameogoza kwa kura 1,568,

Katika Jimbo la Bunda Mjini, Robert Maboto anayetetea kiti chake alipata kura 2,545 na Bulaya alipata kura 625.

Katika Jimbo la Butiama aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia Elimu, Wilson Mahera ameongoza kwa kura 4,295.

Aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini ameshika nafasi ya pili kwa kura 2,341.

Jimboni Rorya, aliyekuwa mbunge, Jafari Chege ameongoza kwa kura 7,866 akifuatiwa na Sango Kasera (4,785), Nyihita Wilfred (1,034), Nchama Wambura (380) na Peter Sarungi (183).

Musoma Mjini aliyeongoza ni Mgore Miraji kwa kura 2,255 huku mpinzani wake wa karibu akipata kura 1,543

Tabora

Katika Jimbo la Nzega Vijijini, aliyekuwa mbunge, Dk Hamisi Kigwangalla ameshindwa kwa kupata kura 1,715 akitanguliwa na Neto Kapalata aliyepata kura 2,570 na Robert Masegere amepata kura 1,635.

Katika Jimbo la Tabora Mjini, Shabani Mrutu ameibuka kidedea kwa kura 6,612 huku aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Emmanuel Mwakasaka akiwa na kura 228. Wengine (idadi ya kura) ni Hawa Mwaifunga (326), Kisamba Tambwe (395), Deusdedith Kanunu (93) na Godbless Mafole (109).

Mbunge aliyemaliza muda wake Nzega Mjini, Hussein Bashe ameongoza.

Jimboni Uyui aliyeongoza ni Shafin Ahmed (5,605) akifuatiwa na Shaban Ntahondi (2,566), Athman Maige (853), Mohamed Hassan (147) na Boniface Semela.

Igalula ameongoza Juma Mustapha (4,056) akifuatiwa na Venance Protace (3,344), John Ntonga (348), Athaman Futakamba (273), Bakari Ramadhan (122) na Mahmud Karatasi (121).

Simiyu

Katika Jimbo la Maswa Mashariki, Dk George Lugomela aliongoza kwa kura 4,759. Aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo na Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo amepata kura 3,088, Dk Adolf Saria (373), George Mayunga (369) na Nyangi Kimori (20).

Jimbo la Maswa Magharibi, aliyekuwa mbunge wake, Mashimba Ndaki ameongoza kwa kura 5,212 akifuatiwa na Dk Zeye Masunga (1,055).

Aliyekuwa Mbunge wa Itilima, Njalu Silanga ameongoza kwa kura 8,285 akifuatiwa na Josephine Makongoro (1,822), Jeremiah Nkulukulu (604) na Emmanuel Subi (248).

Katika Jimbo la Bariadi Mjini, Masanja Kadogosa ameongoza kwa kura 6,969 kati ya kura 7,651.

Jimbo la Bariadi Vijijini, Kundo Mathew ameongoza kwa kura 2,520 akifuatiwa na Lucy Sabu (996).

Kwa upande wa Jimbo la Busega, Simon Songe ameongoza kwa kura 7,787 kati ya kura 10,526 na Dk Raphael Chegeni ameshika nafasi ya pili kwa kura 1,406.

Singida

Jimbo la Iramba Mashariki, Jesca Kishoa ameongoza kwa kura 5,946 kati ya 10,458 akifuatiwa na Francis Mtinga (2,932), Ally Ilanga (526) na aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo, Allan Kiula (446).

Katika Jimbo la Iramba Magharibi, Dk Mwigulu Nchemba amepata kura  10,604 kati ya 12,429 zilizopigwa.

Mbunge aliyemaliza muda wake Singida Mjini, Mussa Sima amepata kura 678 akiwa nyuma ya Halid Ngulume aliyepata 1,146 na Meya wa Manispaa ya Singida anayemaliza muda wake, Yagi Kiaratu ameongoza kwa kura 2,575.

Mbunge aliyemaliza muda wake Jimbo la Ilongero, Ramadhan Ighondo ameshika nafasi ya tatu kwa kura 2,922, aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili, Lazaro Nyalandu (3,637) na  mfanyabiashara maarufu Dodoma, Haiderali Gulamali ameongoza kwa kura 5,024.

Katika Jimbo la Ikungi Mashariki, Thomas Mgonto amepata kura 2,100, Nusrat Hanje (1,918) na Miraj Mtaturu (1,111).

Arusha

Mbunge aliyemaliza muda wake Longido, Dk Steven Kiruswa ameongoza kwa kura 9,064 akifuatiwa na Petro Ngarikoni (1,421), wakili wa kujitegemea Nicolous Senteu (1,128) na Martha Ntoipo (87).

Jimbo la Karatu, Daniel Tlemai ameongoza kwa kura 7,884, Cecilia Paresso (1,341), Patrice Mathay (659), Pantaleo Paresso (142) na Shedrack Qamna (55).

Katika Jimbo la Arumeru Mashariki, Jushua Nassari ameongoza kwa kura 6,678 akifuatiwa na mbunge aliyemaliza muda wake, Dk Daniel Pallangyo (652), Elisa Mbise (650), Profesa Daniel Pallangyo (372), Johnson Sarakikya (312), William Sarakikya (307), Angela Pallangyo (105) na Rose Urioh (55).

Jimboni Monduli, Mbunge aliyemaliza muda wake, Fredrick Lowassa ameongoza kwa kura 7,137 akifuatiwa na Isack Joseph (2,206), Wilson Lengima (952), Shaban Adam (251), Bilihudi Kisaka (41) na Sabaya Alaisheri (21).

Arumeru Magharibi aliyeongoza ni Dk Johannes Lukumay (5,700) huku mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Noah Mollel akiwa na kura 1,971. Wengine ni Noel Severe (1,645), Joel Meidimi (190), Esther Mollel (88) na Henrietta Temu (23).

Kagera

Aliyekuwa mbunge wa Missenyi, Florente Kyombo ameongoza kwa kura 2,979 na kuwashinda Projestus Tegamaisho, Assumpter Mshama, Jackline Rushaigo, Amina Athuman, Nasiru Byabato na Placidius Ndibalema.

Johnston Mtasingwa amepngoza kura Jimbo la Bukoba Mjini kwa kura 1,408 akifuatiwa na Alex Denis (804), Almasoud Kalumna (640), Jamila Hassan (66) na Koku Rutha (44).

Aliyekuwa mbunge wa Bukoba Vijijini, Dk Jasson Rweikiza ameongoza kwa kura 6,465 akifuatiwa na Faris Buruhan (4,619), Fahami Juma (239), Asted Mpita (124), Edmundi Rutaraka (89) na Philebart Bagenda (44).

Mkuu wa vipindi kituo cha televisheni cha Clouds, Dotto Bahemu ameongoza kura Jimbo la Ngara kwa kura 6,855 akifuatiwa na Stephen Kagaigai aliyepata kura 2,344.

Mbeya

Katika Jimbo la Mbeya Mjini, Patrick Mwalunge ameongoza kwa kura 3,360 akifuatiwa na Dk Mabula Mahande (1,133), Sambwee Shitambala (392), Charles Mwakipesile (133), Sophia Malingumu (100) na Elizabeth Maginga (56).

Katika Jimbo jipya la Uyole, aliyekuwa Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameongoza kwa kupata kura 4,830 kati ya 5,140 zilizopigwa akifuatiwa na Dk Seria Shonyera (275) na Emily Sanga (35).

Jimbo la Kyela, aliyeongoza kwa kura 7,960 ni Baraka Mwamengo huku mbunge aliyemaliza muda wake, Ally Mlagila akiwa na 4,917 akifuatiwa na Elius Mwakalinga (2,321) na Paul Mwakajumba (346).

Mbunge aliyemaliza muda wake Jimbo la Rungwe, Antony Mwantona ameongoza kwa kura 3,292 akimshinda mpinzania wake wa karibu, Sophia Mwakagenda aliyehamia CCM kutoka Chadema (1,645).

Wengine ni Dk Samuel Mafwega (1,486), Godfrey Ngwejela (1,404), Richard Kasesela (1,354), Aliko Mwaiteleke (950) na Eliud Mwaiteleke (818).

Masache Kasaka ameongoza kwa kura 5,569 Jimbo la Lupa akifuatiwa na Noel Ntangu (2,854), Geofrey Mwankenja (2,124) na Sara Sompo (141).

Mbunge aliyemaliza muda wake Jimbo la Mbarali, Bahati Ndingo ameongoza kwa kura 7,132 akifuatiwa na Ibrahim Mwakabwanga (5,922), Sela Msigwa (221), Medson Mwambapa (204) na mwanahabari Leonard Mubali (195).

Katika Jimbo la Busokelo, Lutengano Mwalwiba ameongoza kwa kupata kura 2,999 akifuatiwa na mbunge aliyemaliza muda wake, Atupele Mwakibete (2,254), Ezekiel Gwatengile (539), Thobias Andengenye (503) na Rehema Mwasaga (14).

Katika Jimbo la Malinyi mwanahabari Dk Mecktrids Mdaku ameongoza kwa kupata 2,450 akifutiwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Antipas Mgungusi aliyepata kura 1,408.

Imeandikwa na Yohana Shida (Geita), Derick Milton (Bariadi), John Nditi (Morogoro), John Mhala (Arusha), Abby Nkungu (Singida), Shukuru Mgoba (Mbeya) na Diana Deus (Bukoba).

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button