Wabunge wahadharisha Twiga kununua hisa Tanga Cement

WABUNGE wameihadharisha serikali kuhusu nia ya Kiwanda cha Saruji cha Twiga kutaka kununua hisa za Kampuni ya Saruji ya Tanga.

Suala hilo liliibuliwa bungeni na baadhi ya wabunge jana wakati wakichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.

Hata kabla ya mjadala wa bajeti kuanza, awali Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe (CCM) aliomba mwongozo akisema Kiwanda cha Twiga kinataka kununua hisa za kampuni ya saruji ya Tanga.

Advertisement

Mwambe alisema jambo hilo likifanyika, litaruhusu Kampuni ya Twiga kuwa na umiliki wa zaidi ya asilimia 65 kwenye soko hivyo inaweza kuamua bei ya saruji na wazalishaji wengine watapandisha bei ili kuendana naye.

“Ilishatolewa amri na mahakama kulipinga hili, Mahakama ya Ushindani wa Kibiashara lakini sasa hivi linaonekana linataka kurudi tena likajadiliwe sababu wao bado wana interest (maslahi) ya kutaka kununua Tanga Cement, jambo ambalo litakwenda kuongeza mfumuko wa bei ya vifaa vya ujenzi,” alisema.

Mwambe alitaka kupitia mwongozo huo, serikali itoe maelezo kuhusu sababu za kutaka kuruhusu jambo hilo litokee kwa kuwa litaathiri bei ya saruji.

Mwenyekiti wa Bunge, David Kihenzile alisema hoja ya mbunge ilikuwa na maslahi kama kanuni inavyotaka lakini haikufaa kuingia kwenye kanuni ya mwongozo kwa sababu haikutokea mapema bungeni.

Wakati wa mjadala, Mbunge wa Viti Maalumu, Salome Makamba (Chadema) alisema jambo hilo linaweza kuleta shida ya biashara ya saruji nchini.

Salome alidai kuwa mwaka jana Kampuni ya Twiga Cement iliomba kununua hisa za Kampuni ya Tanga Cement na FCC ilifanya tathmini.

Aliomba ofisi ya Waziri Mkuu isimamie suala hilo kwa kile alichosema mwisho wa siku mfumuko wa bei ukitokea kwenye saruji, yatatokea madhara kama ilivyotokea kwenye sukari na mafuta.

Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu (CCM) alisema mwaka 2020 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitoa maelekezo ya kuangalia namna Watanzania walipita katika msukosuko uliosababisha kupanda kwa bei za bidhaa ikiwamo saruji.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *