Wabunge wasema hotuba imesheheni maono ya Tanzania bora

WABUNGE wamepongeza hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuzindua bunge, kwamba imeonesha matumaini mapya ya Tanzania ijayo tajiri na bora Afrika. Tanzania itafikia ubora huo kama Watanzania kwa umoja wao watashikana na kuamua kwa pamoja kuijenga nchi yao.
Wakizungumzia hotuba hiyo katika mahojiano na HabariLEO, walisema Rais Samia amezungumza kama mama akiwahurumia watoto wake. Mbunge wa kuteuliwa, Dk Dorothy Gwajima wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) alisema Rais Samia ni kiongozi anayeenda na wakati na ana maono makubwa kuinua nchi, ndiyo maana pia amewakumbuka vijana na kuwaundia wizara yao.
“Natoa mwito Watanzania kushikana mikono kutekeleza wajibu wao ili maono ya Rais Samia ya Tanzania bora ifikapo 2030 yatimie,” alisema. Naye Mbunge wa Mombo, David Silinde (CCM) alisema katika sekta ya kilimo, Rais Samia amesema ataimairisha mnyororo wa thamani toka shambani, kiwanda cha kuchakata hadi sokoni. “Mkulima anatakiwa kubadili mtazamo na kuwa mwekezaji, ajikite katika kilimo cha umwagiliaji na hivyo akiwekeza fedha zake, zinarudi,” alisema.
Kwa upande wake, Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo (CCM) alisema Rais Samia anaishi na dunia ya leo, anajua mahitaji ya vijana ya sasa wanataka matokeo ya sasa. Hivyo, ameamua kuwezesha kwa kuunda wizara, kuongeza mitaji na kuongeza fursa zao.
“Rais anataka kuwafikisha Watanzania kwenye nchi ya ahadi, kwa kukuza uchumi wa nchi na kuifanya kupitia uzalishaji wa sekta mbalimbali. Kinachotakiwa ni kufanya kazi pamoja na ifikapo 2030, Tanzania itakuwa tajiri miongoni mwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini (SADC),” alisema.
Naye Mbunge wa Kilosa, Profesa Paramagamba Kabudi (CCM) alisema rais anajua wananchi wa wilaya hiyo wanalima nyanya badala ya kuziuza. Hivyo, viwanda vitajengwa kwa ajili ya kuchakata na kupata juisi ya nyanya.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kisarawe, Dk Selemani Jafo (CCM) alisema rais ametoa hotuba ya Watanzania kufikia nchi ya ahadi ifikapo 2030, maadamu watajikita katika uzalishaji na wataongeza ajira katika sekta mbalimbali.



