Buriani Jenista Mhagama 1967 – 2025

MWANASIASA mkongwe aliyewahi kuwa waziri na mbunge kwa miaka 25, Jenista Joakim Mhagama (58) amefariki dunia. Kwa mujibu wa Spika wa Bunge, Mussa Zungu, Jenista ambaye hadi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu alikuwa Waziri wa Afya, amefariki dunia jana Dodoma.
“Kwa masikitiko makubwa, naomba kutangaza kifo cha Mbunge wa Peramiho Mheshimiwa Jenista Joakim kilichotokea leo 11 Desemba, 2025 jijini Dodoma. Natoa pole kwa waheshimiwa wabunge wote, familia ya marehemu, ndugu, jamaa na wananchi wa Jimbo la Peramiho, Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu,” amesema Spika Zungu.
Kutokana na msiba huo, Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Spika Zungu kutokana na kifo cha Jenista. Katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari Machumu, Rais Samia amemuelezea Jenista ni kiongozi makini, mnyenyekevu, mchapakazi na mwenye historia ndefu ya kulitumikia taifa katika nafasi za uongozi ndani ya Serikali na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ametoa pole kwa wabunge, familia ya marehemu, ndugu na jamaa, na wananchi wa Peramiho na kuwaombea moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu. “Ninatoa pole kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu, wananchi wa Jimbo la Peramiho, familia, ndugu, jamaa na marafiki,” alisema Rais Samia.
Awali, kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa X, Rais Samia alieleza kwa miaka 38, Jenista amekuwa mwanachama mahiri wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kiongozi wa vijana, kiongozi wa wanawake, waziri katika awamu mbalimbali na mnasihi wa wengi katika siasa na maisha.
Taarifa za kifo cha Jenista zilisambaa kwa kasi muda mfupi baada ya Spika Zungu kutangaza kifo cha mkongwe huyo ndani ya Bunge. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe alisema taifa limepoteza kiongozi aliyekuwa mwema, mchapakazi na mzalendo. “Ni msiba mkubwa kwa nchi, alikuwa ni mwenye upendo na aliyeacha alama kubwa katika jamii kwa kufanya kazi kwa ushirikiano. Kwa kweli atakumbukwa kwa uchapakazi wake na uadilifu,” alieleza Profesa Shemdoe.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa kupitia mtandao wake wa kijamii amesema Jenista amemaliza mwendo na atavishwa taji. Ameeleza wana Peramiho wameondokewa na mbunge waliyempenda kwa muda mrefu. “Lala salama Mwana-Ruvuma, lala salama Mwana-Peramiho. Umemaliza kazi, utavalishwa taji. Poleni familia, poleni Wanaperamiho kwa kuondokewa na mbunge mliyempenda na aliyewapenda,” alieleza Msigwa.
Mbunge wa Songea Mjini na waziri wa zamani katika Serikali ya Awamu ya Sita, Dk Damas Ndumbaro alisema amepokea kwa mshtuko kifo cha Jenista. Dk Ndumbaro alisema kumbukumbu za mema yake, kazi zake, upendo na utumishi wake kwa watu ndizo zitakazoendelea kuishi na kuwapa matumaini. “Lala salama dada yangu Jenista Mhagama. Taarifa za kifo chako zimenishtua sana, Ruvuma tulikuwa bado tunakuhitaji, Wana Peramiho bado walikuwa wanakuhitaji, na Watanzania bado walikuwa wanakuhitaji dada,” alisema Dk Ndumbaro.

Ameongeza : “Ninaiombea familia kupata faraja, nguvu na utulivu katika wakati huu mgumu. Kumbukumbu za mema yako, kazi zako, upendo na utumishi wako kwa watu ndizo zitakazoendelea kuishi na kuwapa matumaini”. Mbunge wa Katoro, Kija Ntemi amesema Jenista alikuwa kiongozi mchapakazi, mnyenyekevu na mwenye mchango mkubwa katika uongozi wa taifa. “Natoa pole za dhati kwa familia ya marehemu, waheshimiwa wabunge, wananchi wa Jimbo la Peramiho, na wote walioguswa na msiba huu mzito.
Mwenyezi Mungu awape nguvu na uvumilivu katika wakati huu wa majaribu,” alisema Ntemi. Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tabora, Aziza Sleyum Ally alimuelezea Jenista kuwa mchapakazi, mwalimu wa wengi, mzalendo na kiongozi wa kuigwa. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alisema Jenista alikuwa mbunge kwa miaka mingi na alitoa mchango mkubwa katika maendeleo ya mkoa huo, ikiwamo uendelezaji wa Jiji la Dodoma. “Ameutumikia mkoa na taifa kwa moyo wa upendo. Dodoma imeguswa na mengi aliyoyafanya, na mchango wake utaendelea kukumbukwa,” alieleza Senyamule.
Jenista Joakim Mhagama alizaliwa Juni 23, 1967, Ruvuma. Alianza elimu ya msingi mwaka 1976 katika Shule ya Msingi ya Mfaranyaki iliyoko Peramiho na kuhitimu mwaka 1982. Mwaka 1983 alianza elimu ya sekondari katika Shule ya Wasichana ya Peramiho na kuhitimu kidato cha nne mwaka 1986. Alisoma Stashahada ya Ualimu katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu (TTC) Korogwe kati ya mwaka 1987 hadi 1989.
Amefundisha shule mbalimbali kwa miaka sita mfululizo kuanzia 1991 hadi 1997 na kwa miaka mitano mfululizo 1995 hadi 2000 amekuwa Katibu wa Mfuko Maalumu uliokuwa chini ya Ofisa Elimu wa Wilaya ya Ruvuma (Ruvuma DEO-Trust Fund). Kati ya mwaka 1997 na 2000 alifanya kazi Mamlaka ya Mafunzo ya Elimu ya Ufundi Tanzania (VETA). Mwaka 2000 alichaguliwa kuwa Mbunge wa Viti Maalumu na kupitia uzoefu huo 2005 aligombea Jimbo la Peramiho na kushinda.
Amekuwa mbunge wao hadi umauti unamkuta jana mkoani Dodoma. Mwaka 2010, alikuwa Mwenyekiti wa Bunge na mwaka 2014, aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Januari 2015, aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Utaratibu wa Bunge) hadi Serikali ya Awamu ya Nne ilipomaliza muda wake. Katika Serikali ya Awamu ya Tano alihudumu kama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) na kisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) katika Serikali ya Awamu ya Sita.
Agosti 2024, aliteuliwa kuwa Waziri wa Afya hadi kipindi cha kwanza cha Serikali ya Awamu ya Sita kilipokamilisha muda wake Oktoba, mwaka huu. Ndani ya CCM, Jenista alishika nyadhifa kadhaa kwa kipindi kirefu ikiwa Katibu wa Tawi tangu mwaka 1987 hadi 1990 akiwa TTC Korogwe, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM tangu mwaka 1995, Mjumbe wa Kamati Kuu na pia nafasi ya Katibu wa Umoja wa Wanawake (UWT) ngazi ya kata kati ya mwaka 1995 hadi 2000. SOMA: Rais Samia aomboleza kifo cha Jenista



