Wabungea EALA waonya kauli za wanasiasa

Wabunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika (EALA) kutoka Tanzania, wamewataka  wanasiasa na wananchi kutokutumia kauli zinazotishia umoja wa kitaifa na muungano katika kujadili mchakato unaoendelea wa makubaliano kati ya serikali ya Tanzania na Dubai kwenye ushirikiano wa uendelezaji bandari nchini.

Pia wamemuomba Msajili wa Vyama vya Siasa,kufuatilia kwa makini suala hilo na endapo atabaini kuna ukiukwaji wa mahitaji ya sheria hatua stahiki zichukuliwe.

Wakizungumza na wanahabari leo Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wabunge hao wakiongozwa na Dk Abdullah Makame, wamesema kumeibuka maneno kati ya wanasiasa na wananchi kuhusu uwekezaji wa bandari, baada ya serikali kuichagua Kampuni ya DP World.

Amesema kauli zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa na wananchi zinaleta ubaguzi katika muktadha mzima wa muungano ulioasisiwa na hayati Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume.

“Mjadala unaochukua taswira ya ubaguzi hauna afya kwa mustakabali wa Taifa na unaweza kuhatarisha utulivu tulionao kama Taifa, usipomalizwa mara moja una uwezekano wa kuzalisha ladha chachu za muungano na tunapaswa kuulinda hususan kwa viongozi, ambazo nafasi zetu tumezipata kutokana na vyama vya siasa ambavyo vimesailiwa kwa mujibu wa sheria,” amesema.

Naye Mbunge Machanu Ali Machanu, alisema EAC ni ya watu wenye umoja hivyo ni lazima umoja ulindwe kwani kuna watu wanaona wivu dhidi ya ya Tanzania

“Waafrika wote ni ndugu tusibaguane sisi ni wamoja twende pamoja kwaajili ya kuimarisha muungano, ikiwemo umoja wetu ambao baadhi ya watu wanatuonea wivu, hivyo tuendelee kulinda muungano wetu,” amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button