Wachakataji vyuma chakavu waonywa hatari ya mionzi

ARUSHA: WACHAKATAJI wa vyuma chakavu barani Afrika wametakiwa kushirikiana na mamlaka za udhibiti wa mionzi katika kutambua vifaa vyenye mionzi vinavyoingia kwenye biashara zao, ili kuhakikisha vinashughulikiwa kwa taratibu za kitaalamu na kuepusha kuhatarisha afya za wananchi na mazingira.

Wito huo umetolewa jijini Arusha na Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) Kanda ya Kaskazini, Dk. Mikidad Salehe, akieleza umuhimu wa ushirikiano kati ya wachakataji wa vyuma chakavu na mamlaka za udhibiti wa mionzi.

Amesema ni muhimu wafanyabiashara hao kutoa taarifa wanapobaini au kutilia mashaka uwepo wa vifaa vinavyoweza kuwa na mionzi katika bidhaa wanazonunua, ili hatua stahiki za kitaalamu zichukuliwe.

Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za nchi za Afrika kuandaa miongozo na mifumo madhubuti ya kisheria na kitaalamu ya kudhibiti vyanzo vya mionzi vinavyofikia ukomo wa matumizi.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti wa Mabaki ya Mionzi kutoka TAEC, Peter Pantaleo, amesema kifaa cha mionzi kinapomaliza matumizi kwa mtumiaji wa awali haimaanishi kuwa kinaweza kutumiwa na mtu mwingine bila kufuata taratibu za udhibiti na kupata idhini inayostahili.

Akifungua kongamano hilo, Mkurugenzi Msaidizi wa Sayansi na Teknolojia katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Harun Makandi, amewataka wataalamu hao kuandaa miongozo itakayohakikisha vyanzo vya mionzi vinavyofikia ukomo wa matumizi vinasimamiwa kwa usalama.

Kongamano hilo limewakutanisha wataalamu kutoka Tanzania, Kenya, Gambia, Madagascar, Misri, Nigeria, Malawi, Morocco, Comoro, Namibia na Rwanda kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika usimamizi salama wa mabaki ya mionzi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button