Wachambuzi watabiri uchumi kukua, utulivu kisiasa

WADAU wa uchumi na siasa wamesema uchumi wa Tanzania utaimarika zaidi mwaka 2025 kutokana na utulivu uliopo katika uchumi wa dunia huku wakibashiri utulivu wa kisiasa kutawala.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na HabariLEO, wachambuzi wa masuala ya uchumi na siasa walisema kuimarika kwa sarafu ya Dola ya Marekani kulikosababishwa na kuchaguliwa kwa Rais mteule Donald Trump, kumetoa nafasi kwa nchi kuongeza akiba yake ya fedha za kigeni.

Wamebainisha kuwa kikwazo kilichokuwa kikisumbua uchumi wa dunia, ikiwa ni pamoja na wa Tanzania cha Vita ya Urusi na Ukraine kwa sasa hakina nguvu ya kuathiri uchumi wa dunia kwa sababu hata viongozi wa mataifa makubwa wameumizwa na vita hiyo na sasa wanasaka suluhu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti, Sera na Uchumi (REPOA), Dk Donald Mmari alisema kwa kuwa waliokuwa wakichochea Vita ya Ukraine kwa lengo la kuiumiza Urusi, wameumia wao na dunia kwa ujumla, sasa wamegeuka na kutaka vita hiyo kumalizika ili kuokoa uchumi wa dunia.

Alisema kutokana na hali hiyo, ni wazi kuwa mwaka 2025 vita hiyo inaenda kufikia ukingoni ikizingatiwa kuwa Rais mteule Trump aliahidi kuimaliza vita ndani ya siku 100 za mwanzo za uongozi wake.

Aidha, Dk Mmari aliongeza kuwa pamoja na ukweli huo, ni lazima serikali ihakikishe kuwa sera za uchumi zinatekelezwa kwa ufanisi hususani ukusanyaji wa mapato ili kuiwezesha kuwa na fedha ya kutosha ili kujenga miundombinu zaidi ya kiuchumi.

Alisema ingawa uchumi wa taifa unategemea zaidi sekta ya kilimo, utabiri wa hali ya hewa unaonesha mwaka huu kutakuwa na mvua kidogo, lakini alisisitiza kuwa hilo halitaathiri uchumi kutokana na sera ya umwagiliaji iliyoanzishwa na serikali akisisitiza kuwa kilimo ni maji na sio mvua.

“Tumeona Rais Samia amewekeza katika kilimo cha umwagiliaji kwa vijana na kwa kuwa nchi ina rasilimali maji ya kutosha, serikali inatakiwa kuwaelimisha wananchi namna ya kuvuna maji hayo na kuwekeza katika umwagiliaji,” alisema Dk Mmari.

Mtaalamu wa uchumi ambaye pia, ni Mhadhiri wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Haji Semboja alisema hali ya kiuchumi 2025 itakuwa nzuri kutokana na uwiano uliopo kati ya mifumo ya kisiasa, kisera na kitaasisi kuendana na wakati uliopo.

Alisema ili kuendelea zaidi ni vizuri serikali ikaitazama Sera ya Viwanda ya Mwaka 1996 ambayo ndiyo inayotumika hadi sasa, akisisitiza kuwa Tanzania ya 1996 ni tofauti na ya mwaka 2025.

“Suala lingine ni uteuzi wa viongozi wetu lazima uzingatie taaluma, uwezo wa kazi na kujituma kwa mtu ili akawe msaada mzuri kwa Rais Samia badala ya kuteua mtu ambaye anaishia kuwa ‘chawa’ badala ya kuwa mshauri mzuri wa Rais,” alisema Profesa Semboja.

Kwa upande wake, Dk Isack Safari alisema kutokana na kuendelezwa kwa misingi ya kiuchumi kama miradi ya kimkakati kama Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere, Reli ya Kisasa (SGR), Daraja la Kigongo-Busisi na kuimarishwa kwa Kampuni ya Ndege (ATCL) ni ishara kuwa mwaka ujao uchumi utapaa.

Dk Safari ambaye ni mchambuzi wa uchumi na siasa, aliongeza kuwa Watanzania sasa wamejua thamani ya kilimo, hivyo wanachangamkia kilimo cha umwagiliaji, hivyo kuonesha ishara njema kwa ukuaji wa uchumi mwaka huu mpya.

Mchambuzi wa Masuala ya Siasa, Goodluck Ng’ingo alisema malalamiko yaliyosikika kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni msingi wa kukuza uhuru na uwazi wa Uchaguzi Mkuu wa 2025, hivyo kuleta hali ya utulivu wa kisiasa mwaka ujao.

Alisisitiza kuwa hilo litachagizwa na Falsafa ya Rais Samia ya 4R kama alivyofanya katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kuruhusu wale wote walioenguliwa kurudishwa na kushindwa katika sanduku la kura.

Aliongeza kuwa vyama vya vya siasa vina jukumu la kutoa elimu kwa viongozi wao namna bora ya kushiriki katika chaguzi pasipo na kushikwa na sheria za uchaguzi.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button