Wachimbaji Karatu walia na changamoto ya mawasiliano
ARUSHA; Karatu. Wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu mgodi wa Endagen ulioko kitongoji cha Murus, Kata Endabash Wilaya ya Karatu, wameomba kampuni za simu za kiganjani kupeleka huduma za mawasiliano maeneo hayo, ili waweze kufanya kazi kazi kwa uhuru na kujipatia kipato.
Wachimbaji hao wamewasilisha kero hizo kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella alipofika kwenye mgodi huo kwa lengo la kukagua maendeleo ya mradi wa umeme katika eneo la mgodi, mradi unaotekelezwa na serikali kwa usimamizi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco ) kwa gharama ya Sh milioni 300.
Akizungumza Mwenyekiti wa wachimbaji hao, Endagen, Abdul Mwangu, ametaja kero zinazowakabili ni pamoja na ubovu wa miundombinu ya barabara, inayopitika kwa msimu, ukosefu wa majisafi na salama, ukosefu wa huduma za mitandao ya simu, umeme, shule pamoja na zahanati.
Amesema huduma za mawasiliano ya simu katika eneo hilo ni hafifu na pale inapotokea tatizo wanashindwa kuwasiliana kwa haraka kutokana na ukosefu wa mawasiliano.
Ameiomba serikali kuwasaidia kutatua changamoto hizo, ambazo zinakwamisha shughuli zao za kiuchumi, huku wachimbaji hao wakichangia pato la serikali kwa kulipa kodi zote muhimu.
Kwa upande wake Mongella aliagiza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa), Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini(Tarura) na Tanesco kushughulikia changamoto hizo ndani ya mwezi mmoja kuona namna ya kuwawezesha wachimbaji hao kupata huduma hizo muhimu.
“Tanesco itakamilisha mradi huu mwishoni mwezi Novemba, serikali imetoa sh,milioni 300 za kukamilisha mradi huu na umeme utawaka hapa na mtafanya kazi zenu kwa amani,” amesema.