Wachimbaji madini watakiwa waache kulalamika

WAZIRI wa Madini Dk Dotto Biteko, amewataka wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini nchini kuacha kulalamika badala yake wawajibike kuzingatia miongozo, sera, kanuni na sheria za nchi.

Kauli hiyo inakuja kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na viongozi wa wachimbaji wadogo wakiomba serikali kuiangalia upya tozo ya mapato ya asilimia 2 wanayolipa Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA).

Waziri Dk Biteko amesema hayo leo wakati akizungumuza katika hafla ya upandaji miti mkoani Geita, ikiwa ni kampeni ya kitaifa iliyoratibiwa na Shirika la Madini la Taifa (Stamico).

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, inatimiza wajibu wake kuhakikisha wachimbaji wadogo wanaendesha biashara zao  vizuri,  hivyo kwa upande wao watimize wajibu.

Amesema malalamiko makubwa ya wachimbaji yalikuwa ni kukosa risiti za kielektroniki (EFD), wanaponunua huduma na ndiyo maana serikali kupitia wizara ya madini ilipendekeza tozo ya mapato.

“Wachimbaji wenyewe mkaniambia, bora mtuwekee tozo maalum iitwe tozo ya mapato, ili TRA wasitusumbue, hilo sikulibuni mimi, mwaka jana wakaanzisha tozo ya mapato ya asilimia mbili.

“Mheshimiwa Rais akasema hapana hii lazima muende mkakubaliane vizuri, mwaka huu tukawaambia TRA mambo ya kwenda kutengeneza kodi bila kuwafuata wachimbaji wadogo waachane nayo

“Sasa badala ya kujadiliana muone namna bora ya kufanya, mnachukua muda mwingi sana kulalamika, tunachoweza kufanya tunaweza kuiondoa hiyo tozo ya mapato, mjiandae kulipa kodi ya mapato TRA.”

Awali Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo (FEMATA), John Bina ameiomba serikali kutazama upya tozo ya mapato kwa wachimbaji wadogo kutokana na gharama kubwa za uzalishaji.

Mbunge wa Jimbo la Geita mjini, Costantine Kanyasu amesema kodi zinazokwenda kwenye mapato ghafi huenda zikamdhoofisha mchimbaji mdogo, hivyo ni vyema mapitio ya kodi mpya yafanyike.

“Jambo hili linahitaji utafiti mkubwa, linahitaji ushirikiano mkubwa na wadau, hatuna kipingamizi na serikali kuongeza kodi, lakini tunatamani sana kodi ipatikane kwenye sehemu sahihi.”

Habari Zifananazo

Back to top button