Wachimbaji wadogo 250 waongezewa ujuzi Geita

SERIKALI imetoa mafunzo ya kuongeza ujuzi na maarifa kwa wafanyakazi na wachimbaji wadogo wa madini 250 mkoani Geita ikiwa ni sehemu ya kufanikisha adhma ya uchimbaji salama na wenye tija.
Mafunzo hayo yameratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu ikiwa ni utekelezaji wa programu ya kitaifa ya kukuza ujuzi na mnyororo wa thamani katika sekta ya madini.
Akifungua mafunzo hayo yalyofanyika kwa siku tano Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Alana Nchimbi amesema lengo ni kuhakikisha nguvu kazi ya taifa inapata ujuzi, ili iweze kujiajiri na kuajiriwa kwa nia ya kupata nguvu kazi stahiki kwa ufanisi wa kazi.
“Wachimbaji wamefundishwa sheria za madini, matumizi sahihi yakemikali na vilipuzi, kutambua miamba yenye madini, pamoja na namna ya kuongeza thamani kwenye madini.
“Dhamira kuu ni kuwafanya waendane na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ili watoke kuwa wachimbaji wadogo, wawe wachimbaji wa kati na baadaye wachimbaji wakubwa” amesema Alana.

Mjiolojia Mwandamizi kutoka Wizara ya Madini, Joseph Matalu amesema program hiyo inajumuisha mafunzo ya msingi ya ujuzi na vitendo kuhusu mbinu bora za utafiti, uchimbaji na uchenjuaji salama.
Ameongeza pia programu inahusisha mafunzo ya utunzaji wa mazingira, usimamizi wa afya na usalama kazini pamoja na matumizi ya teknolojia sahihi katika shughuli za madini.
Amesema hatua hiyo ni mwendelezo wa kuwakumbusha wachimbaji wajibu wao wa kufuata sheria, kanuni, na taratibu zinazosimamia sekta ya madini kwa ustawi wa sekta ya madini.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati amekiri mafunzo hayo ya nadharia na vitendo yataboresha uzalishaji, kuimarisha na kuhakikisha usalama kazini kwa kuendana na mabadiliko ya teknolojia.
“Katika mwaka huu wa fedha 2024/25 ofisi ya Waziri Mkuu imepanga kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wasiopungua 600 kwenye mikoa ya kimadini ya Geita, Mbogwe na Chunya” amesema Gombati.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Wachimbaji Wadogo Wanawake mkoani Geita (GEWOMA), Asia Masimba amesema mafunzo yameongeza uelewa wa utunzaji taarifa na matumizi sahihi ya teknolojia migodini kwa wachimbaji.