Wadau haki jinai waeleza faida ziara bandarini

WADAU wa haki jinai Mkoa Kigoma wamefanya ziara kutembelea shughuli za mamlaka ya bandari katika Bandari ya Kigoma na Kibirizi ili kuwezesha kuwa na uelewa mpana wa shughuli za bandari iweze kuwasaidia yanapotokea mashauri mahakamani kuhusiana na jambo lolote la kesi za jinai na madai zinazotokea bandarini.
Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Stanslaus Kagisa akizungumza wakati wa warsha ya siku mbili kwa wajumbe wa kamati ya haki jinai Mkoa Kigoma amesema TPA imelifanya jambo hilo kuwapa uelewa na kujua kwa undani shughuli zinazofanywa na taasisi hiyo.
Kagisa amesema kuwa serikali inafanya uwekezaji mkubwa katika bandari zake ikiwemo bandari za Ziwa Tanganyika ikiwemo za Mkoa Kigoma hivyo mabilioni hayo yanaongeza hatari yakuongezeka kwa mashauri ya jinai.
Amesema majaji, mahakimu, wapelelezi, ofisi ya mwendesha mashitaka wanapojua kwa undani shughuli za bandari watasaidia kuharakisha kesi lakini maamuzi yao kuzingatia sheria na hasara inayoweza kupatakana katika uwekezaji huo.
Akizungumza katika warsha hiyo baada ya kupata maelezo ya uendeshaji wa bandari na kutembelea bandari za Kigoma, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Augustine Rwizile amesema mwenendo wa kesi wanazosimamia na hukumu wanazotoa zinazingatia sheria lakini kuwa na uelewa mkubwa wa eneo ambalo kesi inazungumziwa inatoa picha ya hukumu inayostahili kutolewa.
Amesema ziara waliyofanya katika bandari za Kigoma inawapa picha ya namna gani wasimamie kesi hizo kwa uharaka wake na kwa maslahi ya Taifa hasa kwa miradi ya kimkakati kama hii ya bandari hivyo ziara hiyo kwao imekuwa na manufaa makubwa katika kurahisisha utendaji kazi wao.
Mkuu wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Kigoma, Alfred Kasolo amesema kuwa bandari ni eneo la kiuchumi na biashara ambalo linatoa fursa ya upatikanaji wa pesa hivyo kuwepo kwa makosa mengi ya jinai na madai hivyo wao kama wadau wa haki jinai mafunzo na ziara hiyo itakuwa na tija kubwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya upelelezi.



