Wadau kuendelea kushinikiza mabadiliko sheria ya ndoa
MTANDAO wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania (TECMN) umesema wadau wataendelea kushinikiza mabadiliko ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 hususan kwenye vifungu vya 13 na 17 vinavyoruhusu na kutetea ndoa za utotoni.
Pia umeishauri serikali kuhakikisha unatekeleza kwa vitendo sheria ya elimu ambayo inatoa adhabu ya kifungo kwa wazazi wanaowakatisha masomo watoto wao na kushinikiza kuolewa.
Akizungumza na HabariLeo, Mratibu wa TECMN, Lilian Kimath amesema wasichana wengi wanaoolewa hawawezi kuchangia ipasavyo kwenye uchumi wa familia, hivyo kuwa tegemezi kwa wanaume zao.
Amesema utegemezi huo huchangia kuongezeka kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na ongezeko la kaya masikini hususan vijijini.
Amesema wanaamini mabinti wakivunja ukimya na kuwa mstari wa mbele kujisimamia na kukataa ndoa hizo, watakuwa chachu ya kufanya mabadiliko kwenye jamii inayowazunguka.
Kimath ameeleza kuwa viongozi wa dini wana sauti kubwa katika kuielekeza serikali kufanya mabadiliko kwenye sheria ya ndoa.
‘’Viongozi wa dini huleta msukumo wa maadili ya kijamii hivyo kwa kutumia ushawishi wao watatoa elimu juu ya madhara ya ndoa za utotoni na kuwalinda wasichana,’’ amesema Kimath.
Ameongeza kuwa ‘’Tunakabiliwa na mila na desturi kandamizi hususani mikoa ya kanda ya ziwa lakini tunaendelea kutoa elimu kwa jamii ili wasichana hawa waendelee kusoma, wapate elimu afya ya uzazi na kujitambua.’’
Itakumbukwa kwamba Rebecca Gyumi ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative, alifungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu ya Tanzania kwa niaba ya watoto wote walio katika hatari ya kuingia kwenye ndoa za utotoni dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali kupinga vifungu vya 13 na 17 vinavyoruhusu mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14 na 15 kuolewa kwa ridhaa ya wazazi au kwa amri ya mahakama.
Hata hivyo, mahakama hiyo katika uamuzi wake, ilitamka kwamba vifungu vya 13 na 17 vya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ni vya kibaguzi na vinakwenda kinyume cha Katiba na kwamba vimepitwa na wakati.
Kuhusu kuwakatisha watoto masomo, Kimath alisema wazazi huwakatisha masomo watoto wao na kuwataka kuolewa wakiwa na umri mdogo na wengine huwataka kujaza ‘madudu’ kwenye mitihani ili wasifaulu jambo ambalo ni kukandamiza haki ya elimu kwa mtoto.
‘’Sheria ya elimu iko wazi kwamba itatoa adhabu kwa wazazi watakaobainika kuwakatisha masomo watoto wao lakini ni legevu katika maeneo ya vijijini ambako hufichiana siri kutokana na kujuana, hii inasababisha wasichana wengi kuolewa wakiwa wadogo na kukosa haki yao ya kupata elimu,’’ ameeleza.
Amefafanua kuwa mtandao huo utaendelea kutoa elimu kwa wazazi kuhusu umuhimu wa elimu na athari za ndoa za utotoni ambazo huchangia kuwa na kizazi chenye ukosefu wa elimu, kuongezeka mimba za utotoni na vifo vya uzazi.



