KAGERA. Bukoba. Wadau wa mahakama na wananchi kwa ujumla wametakiwa kujifunza na kushiriki katika majaribio ya mfumo mpya wa teknolojia ambao utatumika kuanzia Novemba mosi mwaka huu unaojulikana kama E- Case Management System.
Akizungumza na wadau wa mahakama mkoani Kagera, Jaji Mkuu na Mwenyekiti wa Tume ya mahakama, Profesa Ibrahim Khamis Juma, amesema kuwa mfumo wa Tehama unaotumika Sasa hivi Kama sehemu ya teknolojia ujulikanao kama (GSS2) umezidiwa, lakini tayari mfumo mpya umeanza kufanyiwa majaribio, hivyo ni muhimu kila mdau wa mahakama kushiriki na kuendana na mabadiliko, ambapo karatasi mahakamani hazitatumika tena.
Amesema kuwa Tume ya Mahakama inaendelea na ziara katika mikoa mbalimbali nchini na kukutana na tume za maadili za mikoa na wilaya, ambapo amepongeza Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba kuwa mashauri yote ya mahakamani hapo kwa asilimia 99 wanatumia digitali.
Ametoa wito kwa watumishi kutoa elimu kwa wadau kama polisi, magereza, dawati la jinsia na watu wote wanaofanya kazi na mahakama kujifunza kutumia mfumo wa sasa.
Ameomba kwa serikali kuhakikisha kasi ya umeme unaosambazwa vijijini usiache nyuma mahakama za mwanzo, kwani matumizi ya teknolojia yanahitaji umeme, hivyo watumishi wote na wananchi watalazimika kutumia huo mfumo, ambapo mahakama zote zitapaswa kuwa na huduma ya umeme.
Mfumo huo mpya unatarajia kutumika kufanya usajili wa mashauri mahakamani ,kutunza kumbukunbu za kesi, kutoa hukumu, kukata rufaa na huduma zote za haki ikiwemo kurahisisha muda na kupunguza mashauri haraka mahakamani, ambapo mwananchi atafatilia mwenendo wa kesi yake na kupata taarifa hata kupitia simu janja ya mkononi.
“Tunaendelea kukumbushia maadili ya watumishi wetu wa mahakama, huwezi kutoa haki kama hauna maadili mazuri, mifumo mipya ya teknolojia itarahisisha haki za wananchi na utoaji huduma, ambapo kama mtu hatoridhika atatoa malalamiko yake na tutapata kupitia mfumo.
“Watumishi wetu wanapaswa kuwa weledi na wenye mifano ya kuigwa katika jamii,kutoa haki bila upendeleo,kujali muda, kufanya kazi kwa wakati na haraka na kuhakikisha wananchi wanapata huduma sitahiki, ” amesema.
Akizungumzia matarajio ya Tume ya Mahakama na wadau wa mahakama kamishina wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Jaji Kiongozi Mustapher Siyani amesema kuwa serikali inaendelea kusogeza huduma kwa wananchi na matarajio ya tume hiyo ni kuwa kila tarafa nchini inakuwa na mahakama moja, lengo ikiwa ni kila kata siku za usoni.
Alisema Tanzania ina mahakama 947 Kati ha hizo mahakama 147 hazitumiki kutokana na uchakavu wa majengo na miundombinu, mahakama 212 zinatembelewa na mahakimu hazina watumishi wa kutosha ,mahakama 29 maeneo yake yamevamiwa na wanachi wanaoendelea kufanya shughuli nyingine.
Alisema ili kusogeza huduma kwa wananchi kwa mwaka 2023/2024 mahakama 60 zitajengwa na serikali, akitoa wito kwa wenyeviti wa mitaa na vijiji kulinda maeneo ya mahakama yasivamiwe.