Wadau wakusanyika kujadili upatikanaji maji yaliyo chini ya ardhi

DAR ES SALAAM: TANZANIA imefanya majadiliano ya namna ya kutumia maji, yaliyo chini ya ardhi ili kupunguza mzigo mkubwa wa kutegemea maji yaliyo juu ya ardhi yatokanayo na maziwa, mito, chemichemi, maeneo oevu na bahari.

Majadiliano hayo ni ya siku mbili, na yanajumuisha Serikali ya Tanzania, taasisi za utafiti, taasisi za maji, na wadau wa maendeleo, ambapo yameanza leo na yatahitimishwa kesho Dar es Salaam.

Rosemary Rwebugisa, Mkurugenzi msaidizi anayehusika na utunzaji rasimali maji kutoka wizara ya maji ambaye ameshiriki majadiliano hayo akimwalikisha mgeni rasmi, Katibu mkuu wa wizara ya maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amesema, Tanzania inalenga kupunguza adha ya maji, kwa kuwekeza katika maji ya ardhini kwani maji ya juu ya ardhi yanakumbwa na uchafuzi unaotokana na majanga ya asili, shughuli za binadamu na kuathiriwa na mabadiliko ya tabia ya nchi ikiwemo ukame hivyo maji ya ardhini yatatumika kuziba pengo.

Advertisement

Tanzania inachukua hatua hii ikiwa ni kupanua wigo wa upatikanaji wa maji safi kwa matumizi ya binadamu, kwani vyanzo vya maji vilivyo juu ya ardhi (mito, maziwa, chemichemi, maeneo oevu na bahari) vinakumbana na changamoto nyingi, ikiwemo mabadiliko hali ya hewa na tabia ya nchi, na uchafuzi unaotokana na shughuli za kibinadamu.

Majadililiano hayo yamefanyika Jijini Dar es salaam chini ya mwamvuli wa jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika kitengo cha kushughulikia matumizi na usimamizi wa maji ya ardhini (SADC-GMI).

Malengo ya SADC-GMI ni kufuatilia, kutafiti na kuwekeza katika teknolojia ya kutumia maji ya ardhini ili kuhakikisha upatikanaji wa waji, ikiwa ni kuelekea kutimiza Malengo ya Maendeleo ya Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya 2030, ambapo, lengo namba 6 la Umoja wa Mataifa linahitaji kila mwananchi kuwa na uhakika wa kupata maji safi na salama ifikapo 2030.

Katika majadiliano ya leo, taasisi mbalimbali za ndani na nje ya Tanzania zimeshiriki, zikilenga kujadiili fursa, changamoto na namna ya kupata ufadhili wa kutosha wa kuendesha miradi ya maji ya ardhini kwa ajili ya manufaa ya nchi. SADC-GMI ilianzishwa mwaka 2008 na Afrika Kusini, na baadaye nchi za Tanzania, Malawi na Zambia zilijiunga na mradi huo.