Wadau wataka mazungumzo kumaliza migogoro ya dunia

DAR ES SALAAM: WADAU wa masuala ya amani na viongozi wa dini wameguswa na kile kinachoendelea kati ya Iran, Marekani na Israel na kuzihimiza nchi hizo zinazokinzana kukaa mezani na kufanya mazungumzo ili kumaliza migogoro inayoendelea na kurejesha amani ya dunia.
Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam wakati wa kongamano la kumbukumbu ya kiongozi wa Iran, Ayatollah Sayyid Ali Khamenei, lililowakutanisha viongozi wa dini, wanazuoni na wananchi kujadili umuhimu wa kulinda amani duniani.
Ayatollah Sayyid Ali Khamenei alikuwa Kiongozi Mkuu wa Iran kuanzia mwaka 1989 hadi 2026, na alikuwa mtu mwenye mamlaka makubwa zaidi katika mfumo wa uongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kabla ya kuuawa Februari 28, 2026, kufuatia mashambulizi ya kijeshi yaliyofanywa na Marekani na Israel.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Sheikh Alhad Mussa Salim, amesema dunia inapaswa kuelekeza nguvu katika mazungumzo badala ya kuendeleza migogoro inayohatarisha usalama wa kimataifa.
Amesema migogoro inayoendelea sasa si ya Mashariki ya Kati pekee bali ina athari kwa dunia nzima, hivyo mataifa yanayokinzana yanapaswa kukaa pamoja na kujadiliana ili kupata suluhu ya kudumu.
“Tunapenda kuona dunia inatawaliwa na amani. Migogoro inayoendelea inaathiri dunia nzima, hivyo ni muhimu kwa mataifa yanayotofautiana kukaa na kuzungumza ili kurejesha amani,” amesema.

Kwa upande wake, Balozi wa Iran nchini Tanzania, Mohamed Javad, amesema kongamano hilo limewakutanisha watu kutoka makundi mbalimbali ya kijamii na dini kuomboleza kifo cha kiongozi huyo wa kiroho na kuonesha mshikamano.
“Ninapenda kuwashukuru wananchi na Serikali ya Tanzania kwa namna walivyotuunga mkono katika kipindi hiki kigumu. Watu wengi walifika katika makazi ya ubalozi kutoa pole na faraja kwa watu na Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran,” amesema.

Naye Mchungaji Canon Mstaafu Askofu Dk. Isaya Mugaragu wa Kanisa la Anglikana Tabora amesema tukio hilo ni la huzuni kubwa kwa watu wa dini zote kwa kuwa kifo cha kiongozi huyo kimetokea katika mazingira yasiyotarajiwa.
Amesema dunia inapaswa kuheshimu sheria za kimataifa zinazokataza taifa moja kuingilia uhuru wa taifa lingine au kutumia nguvu zake kulinyanyasa taifa jingine.
“Kwa mujibu wa misingi ya Umoja wa Mataifa hakuna taifa linalopaswa kuingilia taifa lingine au kutumia nguvu au uchumi wake kuwadhulumu wengine. Amani ndiyo msingi wa maendeleo ya dunia,” amesema.
Aidha amewataka Watanzania kuendelea kulinda amani ya nchi yao na kuhakikisha yeyote anayetaka kuvuruga utulivu anachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Mwalimu na Mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Al-Mustafa Tanzania, Ghawth Nyambwa, ameseema Ayatollah Khamenei pia alisisitiza uzalendo na kuwahimiza vijana kuipenda nchi yao ili kulinda misingi ya amani na usalama wa taifa.
Kwa upande wake, Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania, Hemed Jalala, amesema kumbukumbu za kiongozi huyo zina umuhimu mkubwa kwa Watanzania kutokana na historia ya mahusiano mazuri kati ya Iran na Tanzania.
Amesema kiongozi huyo alijulikana kwa kuhimiza umoja na mshikamano wa Waislamu pamoja na kusisitiza mazungumzo kama njia ya kudumisha amani duniani.
Naye, Naibu Waziri wa zamani wa Viwanda, Shamimu Khan, amesema anasikitishwa na vifo vya mamia ya wanafunzi wasichana nchini Iran na kusisitiza umuhimu wa mazungumzo kati ya pande zinazohasimiana ili kuokoa maisha ya watu wengi wanaopoteza maisha au kuteseka kutokana na migogoro.



