Wafamasia watakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya dawa
DAR ES SALAAM: MFAMASIA Mkuu wa Serikali, Dk Daudi Msasi, amewataka wafamasia nchini kubadili mtazamo wa taaluma yao kwa kuangalia zaidi matumizi sahihi ya dawa na matokeo ya matibabu kwa mgonjwa, badala ya kujikita zaidi katika kuhakikisha dawa zinapatikana.
Dk Msasi amesema hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafamasia Duniani, yanayofanyika kila Septemba 25, sambamba na Kongamano la Wafamasia na wadau wa sekta ya dawa.
Amesema pamoja na kuendelea kuhakikisha upatikanaji wa dawa, wafamasia wanapaswa kuangalia kama mgonjwa anapata dawa sahihi, kwa dozi inayostahili na kwa muda unaotakiwa, pamoja na kufuatilia iwapo matumizi ya dawa hizo yanaleta matokeo yaliyokusudiwa.
“Tunapaswa kujiuliza kama mgonjwa anapata dawa sahihi, kwa dozi sahihi na kwa muda sahihi, lakini pia tuangalie kama matumizi ya dawa hiyo yanaleta matokeo yaliyokusudiwa,” amesema Dk Msasi.
Amesema taaluma ya famasia inapaswa kwenda zaidi ya usimamizi wa dawa na kujikita katika kujenga mifumo inayohakikisha wagonjwa wanapata huduma salama, sahihi na kwa wakati.
Dk Msasi pia amesisitiza umuhimu wa wafamasia kuendelea kujisomea na kuongeza uelewa kuhusu dawa wanazozisimamia ili waweze kutoa huduma bora zaidi kwa wagonjwa.
Aidha, amesisitiza utekelezaji wa Clinical Pharmacy Services (CPS) katika vituo vya afya, akisema huduma hizo zitasaidia kuweka mwongozo wa namna wafamasia wanavyopaswa kushiriki katika huduma za wagonjwa na kuhakikisha uwepo wa ufanano katika utoaji wa huduma kutoka kituo kimoja cha afya hadi kingine.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania, Fadhili Ezekia, amesema maadhimisho hayo kupitia kongamano hilo yanatoa fursa kwa wataalamu na wadau kujadili namna mfamasia anavyoweza kushiriki zaidi katika huduma jumuishi za afya ili kuboresha matokeo ya huduma kwa wananchi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Christian Social Services Commission (CSSC), Peter Maduki, amesema taasisi hiyo inashiriki katika kuimarisha taaluma ya famasia nchini kwa kutoa mafunzo katika vyuo vya famasia vya serikali na binafsi.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha taifa linapata wafamasia wenye uwezo na ujuzi unaohitajika katika kutoa huduma bora za afya.
Maadhimisho ya Siku ya Wafamasia Duniani mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu: “Kuwawezesha Wafamasia kwa Mustakabali wa Kesho Bora.”



